top of page

Jinsi tunavyoweza kuelewa lugha ya upendo ya watoto wetu.

  • C-Sema Team
  • Mar 11
  • 3 min read

Watoto wanayo lugha yao maalum ya kuelezea upendo wao kwa watu wanaowazunguka, japo ni nadra kwa watu kuelewa lugha hiyo. Watoto wetu wanatupenda kwa dhati, hata kama hawawezi kila mara kueleza hilo kwa maneno ama kuonesha kwa vitendo. Kuelewa lugha yao ya upendo kunaweza kusaidia kuimarisha uhusiano wetu nao na kuwafanya wajihisi salama na kuthaminiwa.

Dhana ya Dr. Gary Chapman kuhusu lugha tano za upendo ambazo ni mguso wa mwili, maneno ya kuhimiza, muda wa pamoja, zawadi, na vitendo vya huduma—inaweza kutumika kwa watoto pia. Kuelewa lugha yao ya upendo hutusaidia kuungana nao kwa njia inayoeleweka zaidi kwao.


Kama ilivyo ata kwetu watu wazima, watoto pia huonesha upendo wao kwa njia mbalimbali, hata kama si kwa maneno ya moja kwa moja. Wanaweza kutafuta ukaribu wa kimwili kwa kukumbatia au kushikana mikono, kutabasamu na kucheka tunapokuwepo, au hata kuiga tabia zetu kama ishara ya upendo wao. Pia, wanapotuangalia machoni kwa furaha au kutuletea zawadi ndogo ya vitu vyao wanavyovipenda kama mchoro au mdoli, wanadhihirisha hisia zao za upendo. Wakati mwingine, watoto huonesha upendo kwa kutamani muda zaidi pamoja nasi au kutafuta faraja wanapokuwa na huzuni.


Lugha tano za upendo kwa watoto

Kila mtoto ana njia yake ya kipekee ya kueleza na kupokea upendo. Kutambua hili hutusaidia kukuza uhusiano wa kina wa kihisia na watoto wetu:

Mguso – Watoto wanaopendelea lugha hii hupokea na kueleza upendo kupitia kukumbatiwa, kubembelezwa, na kushikana mikono. Ishara kama kuguswa mgongo (back pats) kwa upole au busu la usiku mwema huwafanya wajihisi salama na kupendwa.

Maneno ya kuhimiza na kutia moyo – Sifa na maneno ya kutia moyo kama "Tunakupenda," "Najivunia kuwa na mtoto kama wewe," au "Wewe ni wa pekee" au kumpigia makofi na kumshangilia kwa furaha anapofanikisha jambo huongeza kujiamini kwa mtoto na kumfanya ajihisi kuthaminiwa.

Muda wa Pamoja – Watoto wanaothamini lugha hii wanapenda kushiriki nasi muda wa pekee, iwe ni kwa kucheza, kusoma pamoja, au mazungumzo ya ana kwa ana. Umakini wetu kwao tukiwa pamoja hasa kujali, kusikiliza na kuonesha ushirikiano  hujenga uhusiano mzuri wa kihisia.

Zawadi (gifts)– Watoto wanaopokea upendo kupitia zawadi huthamini hata ishara ndogo kama kadi yenye ujumbe wa upendo. Kinachoangaliwa zaidi si thamani ya zawadi, bali nia iliyo nyuma ya hiyo zawadi.

Vitendo vya huduma – Watoto hupenda kuonesha upendo kwa kushiriki kusaidia kazi hata kama hawaziwezi kwa ufanisi, hivyo kumuonesha ushirikiano kwa kutomkatisha tamaa na kumsaidia mtoto kwenye kazi za shule, kumpikia chakula anachopenda, au kumrekebishia mdoli  iliyovunjika ni njia za kuonesha upendo kwa vitendo badala ya maneno.


Kila mtoto ana lugha moja kuu ya upendo, lakini anaweza pia kuthamini vipengele vya lugha zingine. Tunaweza kugundua lugha yao ya upendo kwa kuchunguza tabia zao:

  • Je, wanapenda kukumbatia/kukumbatiwa au kushikwa mikono? (Mguso wa mwili)

  • Je, wanapenda kusikia maneno ya kutia moyo? (Maneno ya kuhimiza)

  • Je, wanapenda kuwa na muda wa pekee na sisi au marafiki zao? (Muda wa pamoja)

  • Je, wanapenda kutuletea zawadi ndogo au kupokea zawadi? (Zawadi)

  • Je, wanapenda kutusaidia au kusaidia wenzao katika shughuli ndogo ndogo? (Vitendo vya huduma)


Kuelewa ishara hizi hutusaidia kujenga uhusiano wa kina wa kihisia na watoto wetu. Ni muhimu pia kuelewa kuwa lugha ya upendo ya mtoto inaweza kubadilika kadri wanavyokua. Kuwa makini na mabadiliko haya huhakikisha kuwa wanahisi kupendwa na kuthaminiwa kila wakati.


Hivyo basi tujifunze kuwasiliana katika lugha yao ya upendo, ili tujenge msingi thabiti wa uhusiano uliojengwa kwa imani, usalama, huruma na upendo. Watoto wanaojua wanapendwa hukua kujiamini, kuwa na huruma, na hisia za kuthaminiwa.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

 

 

 

 

 

 

bottom of page