top of page
  • Faith Mkony

''Pedophile'' ni nani? na ana tabia zipi?

Updated: Aug 31, 2023

Mtu mzima anayependa/kuvutiwa kufanya mapenzi na watoto wadogo, kitaalamu anajulikana kama pedophile kwa lugha ya kiingereza.



Hii ni hali ya kiafya ambayo inamfanya mtu mzima kuvutiwa kufanya mapenzi na watoto ambao hawajafikia umri wa kubalehe. Hakuna wasifu thabiti wa kumtambua ‘’pedophile’’, mtu yoyote kijana au mzee, mwanaume au mwanamke anaweza kuwa na tabia hii.


Ila kwa ujumla, pedophile huwa na tabia ya kujitenga na watu wazima na kufurahia zaidi kuwa na watoto. Hujenga uhusiano na urafiki wa karibu na watoto walio karibu nao na huwa na mbinu za kujenga urafiki na watoto kiurahisi.


Watu wenye tabia hii mara nyingi hujaribu kuwarubuni watoto kwa kutumia vitu kama zawadi, pesa, michezo ya video, na vitu vingine vya kuchezea ili kuwashawishi kufanya nao mapenzi, kuwashika maungo yao ya siri au kuwapiga picha/video wakiwa watupu.


Pedophile hatumii nguvu au kuwalazimisha watoto kujihusisha kingono, ataanza kwa kujenga uaminifu na urafiki kwa mtoto kisha ataanza kumgusa mwili, kumbeba au kumpakata, kumbusu, kumtomasa, kumshawishi mtoto amshike sehemu zake za siri na kadhalika.




Pedophile pia anaweza kukusanya na kuhifadhi picha mnato na picha mwendo za watoto wakiwa uchi au zinazoonyesha sehemu zao za siri.


Vile vile wanaweza kutumia fursa yakua karibu na watoto kutengeneza hizi picha bila kuwashika au kuwaingilia kimwili, picha hizi anaweza kuzitumia mwenyewe au kuzisambaza mtandaoni kwa ajili ya wengine wenye tabia kama yeye kutumia au hata kuziuza kwa kujinufaisha.

Pedophile hutumia fursa ya hali ngumu ya kimaisha au malezi kuwapata watoto. Mara nyingi watoto ambao wanaonekana kuhitaji upendo huwa kwenye hali hatarishi zaidi kurubuniwa na pedophile.




Mara nyingi (lakini sio zote) pedophile huwa ni wanaume, wanaoonekana kuwa watu wakawaida wanaokaribia miaka thelathini na zaidi. Watu hawa huchagua kazi ambazo zinawapa nafasi kubwa ya kuwa karibu na watoto ili waweze kutimiza matakwa yao. Watu hawa huwa wana familia, hawana rekodi ya uhalifu, na hukanusha kwamba wanawadhuru watoto, hata baada ya kukamatwa, kuhukumiwa na hata kufungwa.

Ndoa zao mara nyingi zina matatizo ya kimapenzi, na hutumika kama kizugio cha matamanio yao ya ukweli na wengine hawana ndoa kabisa au huwa na uhusiano na wanawake wanaoonekana kutokua na afya nzuri ya akili.


Hata kama hawana watoto, Pedophile wana tabia ya kuweka vitu nyumbani kwao vinavyowavutia watoto (kulingana na umri wanaoupendelea) ili kuwafanya watoto kuja nyumbani kwao na kuwafanya warudi tena na tena.



Pedophile anaweza kuwatafuta watoto wa kuwafanyia ukatili peke yake au kwakutumia vikundi vya mitandao ya jamii. Mara nyingi mtu huyu alikuwa muhanga wa aina fulani ya unyanyasaji wa kingono utotoni ingawa haijathibitishwa kitaalamu kua mhanga wa ukatili wa kingono utotoni atakuja kuwa mtu mzima anayewafanyia watoto ukatili.


Pedophile anaelewa kuwa tabia hizi hazikubaliki katika jamii na ni kinyume na sheria ya nchi hivyo huwa wanazingatia usiri wa hali ya juu na kutumia mianya ya malezi hasi kutimiza malengo yao. Ni muhimu kuelewa kuwa, haimaanishi kwamba kila mtu ambae anapenda kuwa na ukaribu na watoto ni pedophile.


Ila, mtoto akikutaarifu kuwa rafiki, jirani, mwana familia akiwemo baba, mama, kaka, dada, mjomba au mtu mzima yoyote unayemwamini/anayeaminika kwenye jamii amemgusa sehemu zake za siri/ amampiga picha akiwa mtupu au kumfanyia ukatili wa aina yoyote ni jukumu lako kama mzazi au mlezi kufuata sheria na kutoa taarifa Dawati la Wanawake na Watoto la Polisi, Kituo cha Mkono kwa Mkono au piga Huduma ya Simu Kwa Mtoto kwa kupitia number 116 bila malipo.




Usipuuzie wala usinyamaze kimya, ulinzi wa watoto ni jukumu la kila mwanajamii!! #Malezi

9 views

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page