top of page
  • C-Sema Team

Njia tano za kufanya nyumbani eneo la elimu kwa mtoto

Utakubaliana nasi kuwa 'shule' ya kwanza katika maisha ya mtoto ni nyumbani 'wazazi, ndugu wa familia tandaa, majirani na marafiki wa familia husika.' Jukumu la malezi linatoka kwa Mungu na mzazi hana budi kulitekeleza maadam ameamua kumleta mtoto duniani. Kupitia mzazi/mlezi mtoto anapata nyenzo zitakazoongoza maisha yake yote heshima, utii, unyenyekevu na nidhamu. Yaani wema au ubaya wa mtu mara nyingi ni matokeo ya aliyojifunza nyumbani.


Njia tano za kufanya nyumbani eneo la elimu kwa watoto

Nyumbani ndiko msingi hujengwa. Bahati mbaya 'ualimu' wa nyumbani unatokana na matendo zaidi ya maneno. Mtoto uko naye kila uchao hivyo badala ya kutumia muda mwingi kutoa maelekezo ya tabia njema. Ishi kwa mfano. Unamwambia mtoto sala na ibada ni muhimu katika maisha, wewe unasali? Je, mnahudhuria ibada pamoja?


Kupitia maisha unayoishi utamjengea mtoto misingi ya kiakili na kiimani ili kama ilivyo kwa chakula bora awe na uwiano sawia katika maisha. Bahati mbaya wazazi/walezi wengi huingia katika shughuli hii wakiwa ndiyo kwanza bado vijana. Lugha za ujana na misemo iliyo mingi huwa bado inazo chembe za utovu wa nidhamu. Ukiwa mzazi mtoto anakusikia, anakuiga. Chagua maneno.


Fursa ya kujenga tabia/kukuza vipaji. Anapotoka tumboni mwa mama, mtoto huwa na kurasa zilizo wazi pasi na tabia za aina iwayo-yote. Isipokuwa kwa vipaji na tabia za kurithi mzazi/mlezi wewe unalo-jukumu la kuumba tabia na kukuza vipaji vya mtoto. Ukiwa kama mwalimu wa kwanza wa motto, mwandae kwa ajili ya elimu ya shule (awali, msingi, sekondari, nk.) na stadi za maisha. Muache mtoto ajifunze shughuli tofauti kutoka kwako kulingana na kipaji ulichojaaliwa, shiriki shughuli za jamii ili ajifunze uwajibikaji kutoka kwako.


Umoja wa wazazi/walezi ni wa lazima. Baba na mama wawe wamoja katika kulea. Pale inapotokea tofauti baina yao kuhusu namna ya kutoa maelekezo kwa mtoto basi na wasibishane mbele za mtoto. Ikiwa kwa mfano mama anamwadhibu mtoto na baba hakubaliani na adhabu inayotolewa muombe mama faraghani na mzungumze juu ya hili. Ukomavu namna hii utasaidia kutomchanganya mtoto na jumbe zinazokinzana. Kamwe msikwaruzane mbele za watoto. Tofauti zenu zivumiliwe mpaka mpatapo faragha mbali na watoto. Elimu ianze umri gani hasa?


Elimu inaanza akiwa tumboni kupitia mazungumzo ya mama mtoto anaandaliwa kuzijua sauti za watu wake wa karibu kama baba, mashangazi nk. Hii inakwambia kwamba malezi yanaanza mara tu uwapo mjamzito. Punguza ugomvi usio-lazima na ikiwezekana jenga mazingira rafiki kwa kuwa mwenye furaha wakati mwingi. Mara tu unapomtia mikononi mwako kichanga wako anza kumsemesha. Elimu ya lugha unayotumia ndiyo lugha atakayoanza kuifahamu. Jenga msamiati wenye lugha za staha ili mtoto naye ajifunze hivyo.


Jifunze miongozo ya malezi. Sote tunafahamu kuwa malezi hayana shule eti ukajifunze upate kujua mbivu au mbichi. Nyakati nazo zimebadilika na watu hasa waishio mijini hawakai pamoja na familia tandaa. Hii inamnyima mzazi mpya fursa ya kupata maelekezo ya namna bora ya kulea toka kwa wazazi wazoefu. Pamoja na changamoto hizi, zipo fursa za kujielimisha kupitia vitabu, majarida na makala mfano wa haya. Fursa nyingine adhimu ni mtandao wa intaneti wenye maandiko ya kitaalamu na toka kwa wazazi wa matabaka, makabila na lugha mbalimbali kote ulimwenguni. Jisomeshe.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

1 view

Recent Posts

See All

Comentários


bottom of page