top of page
  • C-Sema Team

Njia 7 za kumwepusha mtoto 'kuharibikiwa' msimu huu wa likizo


Inasikitisha kuona ingawa dhamira zetu ni nzuri kwa kuwapa watoto watakayo msimu huu, sisi wazazi ni sehemu ya tatizo pale watoto wanapoharibikiwa kadri wanavyokua. Tunakusogezea njia muhimu saba unazoweza kutumia kumwepusha mtoto kuharibikiwa.

  1. Mfundishe kuridhika. Mtoto akiridhika na alichonacho hawezi kutamani/kudai asivyonavyo. Mtoto wa umri wowote anaweza kujifunza kushukuru kwa zawadi aliopewa, kuridhika nayo na kuzoea kusema asante. Mtoto anayefahamu mambo haya ni vigumu kuyumbishwa na tamaa kwani anajisikia fahari kwa yale aliyonayo.

  2. Jenga misingi ya zawadi kwa familia. Namna bora ya kudhibiti matarajio ya mwanao ni kujiwekea sababu za kupeana zawadi. Kwa mfano, mnaweza mkajipangia kuwa zawadi iwe mojawapo ya hizi: "kwa ajili ya kuvaa, kwa ajili ya kusoma na hitaji maalumu." Vinginevyo hakuna zawadi. Vievile zawadi si lazima inunuliwe, unaweza mwandikia, umchoree picha ama umtengenezee zawadi. Namna hii utamfundisha kuwa zawadi si lazima itoke dukani kwa fedha bali ni ishara ya upendo toka kwako.

  3. Wekeza muda. Likizo ni wakati mzuri wa wewe kuweka mambo mengine yote pembeni ukatulia na mwanao. Amini usiamini, anataka mawazo yako yasiyogawanyika zaidi ya zawadi unazohangaika nazo. Unapopata muda wa faragha na mtoto unaimarisha uhusiano wa kihisia kati yenu na kupata ushirikiano mkubwa toka kwake. Zaidi ya yote, mtoto atajifunza kwamba furaha hutokana na kukaa pamoja na uwapendao si kushinda madukani (mkinunua zawadi).

  4. Usihofu kutomridhisha. Wazazi mara nyingi tunahamu ya kuifanya dunia kuwa mahali pazuri kwa watoto wetu. Kama kumnunulia simu dhidi ya dhamira zetu au kupika mboga saba tofauti kila mlo ili mtoto aweze kuchagua ale nini aache nini, n.k. Alimuradi tu mtoto aneemeke! Kwa bahati mbaya, wakati sisi tunaondoa 'matuta' ili watoto wapete, tunawafundisha kuchukulia maisha kirahisi bila kujua tunawanyima uzoefu muhimu ambao 'ugumu' wa maisha unaweza kutufundisha (ujasiri, uvumilivu, utayari kukabili changamoto). Lakini nini cha kufanya wakati mtoto akikupandishia mabega kwa kutaka bwerere hizi? Kuwa jasiri: MPUUZE. Punde si punde, mtoto wako atajifunza kwamba maisha yanazo changamoto na kwamba hazitatuliwi kwa kupandisha mabega na kudeka.

  5. Fundisha matumizi ya fedha. Sote tunajua pesa hazichumwi kwenye miti - ama kwenye pochi zetu - Je mtoto wako anajua hili? Ufunguzi pochi kwa kila analodai/anachotaka mtoto ni kitovu cha uharibifu. Unamwambia, utapata utakacho wakati wowote. Badala yake na kwa kuzingatia umri wa mtoto, toa posho za wiki ama mwezi zenye malengo kumfundisha kuachana na matumizi yasiyo ya lazima, kama midoli/mwanasesere, kwenda sinema na marafiki, n.k. Ikiwezekana haya ajifunze kuyagharimia kutokana na kubana matumizi katika posho yake.

  6. Mpe majukumu. Mara kadhaa tunajikuta tunawafanyia watoto kila kitu hata mambo wanayopaswa kutekeleza wenyewe. Kumfungia kamba za viatu (Baby Class) hadi 'kumwomba' mwalimu arekebishe daraja lake la Fizikia (A' Level). Hata kama tuna nia njema, hapa tunamfundisha uzembe - kwamba yupo mtu wa kufanya majukumu yake. Mpangie majukumu na mfunze kujisimamia, namna hii atakuwa mtu wa kuwajibika.

  7. Toa adhabu stahiki pale wanapokosea. Moja ya tabia walizonazo watoto waloharibikiwa ni kudhani kwamba taratibu na sheria kamwe haziwagusi. Tunawajengea nadharia hii kwa kutowafundisha gharama za kutotii sheria/taratibu. Mbaya zaidi ni pale tunaposhindwa kutoa adhabu stahiki wanapokosea. Badilika leo, toa makatazo na yafuatilie na adhabu kulingana na umri wa mtoto.

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org


1 view

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page