top of page
  • C-Sema Team

Nini kifanyike kwa mtoto aliye na tabia ya kuandika katika vitu vya thamani.

Baadhi ya watoto wetu wana tabia ya kuandika juu ya vitu vya thamani, ukutani na kwingineko. Tabia hii inaleta ukakasi na magomvi yasokwisha baina ya watoto hawa na wazazi / walezi wao. Baadhii ya wazazi / walezi wanadhani huenda mtoto mwenye tabia hii ni mtukutu asiyependa kusikia maonyo. Hivyo katika makala haya tumefuatilia kujua iwapo pana ushahidi wa kitaalamu katika tasnia ya malezi kufafanua tabia hii.



Kwanini watoto hufanya hivi? Nini tufanye kuwazuia?

Tumebaini kwamba mtoto mwenye tabia ya kuandika kwenye vitu vya thamani ukutani na kwingineko hufanya hivyo kukata kiu yake ya kujifunza. Yaani sasa amekwenda shule lakini hana nyenzo za kujifunzia nyumbani. Nyenzo kama karatasi, penseli za kawaida na zile zenye rangi mbalimbali za kuchorea na kadhalika. Inashauriwa kwamba mtoto anapoanza kujua kuandika sisi wazazi tunalo jukumu la kuandaa mazingira nyumbani kumkata kiu ya kujifunza.


Mtoto anapojua kusoma anatamani mzazi ujue kuwa anajua. Tunakubaliana kwamba binadamu awaye-yote ni mtu wa 'tambo'. Mshawasha wa kutaka kujionyesha kuwa anajua unapomkumba mtoto hana namna ya kujua 'uthamani' wa anapoandika. Jibu hapa ni kwako mzazi kutenga muda wa kukaa naye akiwa anaandika ama kwenye karatasi, chini ardhini au sehemu nyingine ulomwandalia. Tumia muda huu pia kutuliza mshawasha wake ukimwelekeza anapokosea. Namna hii kiu yake ya kutaka 'uone' anajua itapoa.


Unaposhuhudia mtoto amefanya kitendo hiki badala ya kufoka na kamkaripia na pengine kumchapa viboko, mpe vitendea kazi. Makaripio na viboko vitamletea uoga na kuua ari na mshawasha wa kutaka kujua zaidi. Nidhamu ya uoga inaua udadisi. Yaani kutoka katika 'fahari' wa kujua mpaka kaonekana 'mtukutu alojaa ujinga'. Lazima mtoto achanganyikiwe na chembe nyingi za uthubutu unazizima mapema kabisa maishani. Sasa anakuwa mtu wa kusubiri aambiwe nini sahihi na nini si sahihi. Ndoto za mafanikio yake za kibunifu nazo unazizikilia mbali.


Ikumbukwe zamani hapa Tanzania ili mtoto aanze shule ilimlazimu afaulu 'mtihani' wa kushika sikio lake la upande wa pili. Asipoweza anarudishwa nyumbani. Leo katika zama za sayansi na teknolojiya mtoto anapelekwa shule ya awali hata kabla ya kutimiza umri wa miaka mitatu na ifahamike kwamba hiki ni 'kipindi cha umri wa kuuliza maswali mengi yasiyo na idadi kwa mzazi au mlezi wake'. Msikilize. Mpe macho akuonyeshe ubunifu. Usizime ndoto zake.


Msaidie kujua 'uthamani' wa vitu usivyotaka aandike kwa kukubaliana naye kuwepo kwa ukomo / mipaka ya kujifunda kuandika. Atafahamu kwamba 'hata kama najua', lazima niandike katika mahali sahihi. Jaribu zoezi hili na matokeo yake yatakushangaza. Watoto ni wasikivu mno wakishirikishwa kujua kosa.


Dhamiria kuwekeza katika nyenzo za kujifunzia kwa mfano ubao nyumbani, madaftari, kalamu na vitabu vya hadithi. Nyenzo hizi zitamkata kiu ya kuandika-andika kokote. Mwisho, fanya ufuatiliaji yakinifu. Ukaribu wako kwa mtoto ni muhimu kwake kujua namna bora ya kujifunza.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

5 views

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page