top of page
  • C-Sema Team

Ninawezaje kumfanya mtoto wangu kupenda kunywa maji?

Sote tunajua kuwa maji ni muhimu kwa afya ya mtoto. Maji hupoza mwili na husaidia kulinda joto la mwili, huzuia kuvimbiwa na maambukizi ya njia ya mkojo - yote haya bila kuongeza chochote ndani ya maji (bila chunvi au sukari). Lakini namna gani ikiwa mtoto wako hapendi maji? Makala haya yanakupa njia wanazotumia wazazi wengine kuwapa watoto wao maji kama walivyonukuliwa na mtandao wa Baby Centre.Maji yawepo muda wote. Kila wakati napohisi mwanangu ana kiu, mimi humpa maji. Mara nyingi atanijibu kuwa hana kiu, lakini ninamuomba walau kumnywesha matone matano. Mara nyingi mbinu hii humsaidia kunywa zaidi ya ninavyotaka. Mara tu anapoanza kunywa maji mtoto hugundua kumbe alikuwa na kiu, hivyo hunywa maji mengi zaidi ya yale matone matano. Daima weka kikombe cha maji ya kunywa karibu na mahala mtoto anapopenda kucheza. Mahala anapoweza kuyafikia wakati wowote hivyo atashawishika kunywa maji apatapo kiu.


Chezeni mkinywa maji. Watoto wengi hupenda kushindana na wazazi wao kufanya mambo mara kadhaa. Fanya unywaji wa maji sehemu ya mashindano hayo. Unaweza kujaza glasi ya maji baada ya chakula na kumtaka mtoto kushindana nawe kumaliza glasi yake. Namna hii atakunywa maji pasi kujua lengo lako la kumjenga kupenda maji ya kunywa. Watoto hasa wa mijini unaweza kumwekea mrija katika glasi yake na kumruhusu kunywa maji kwa mrija. Haka ka-mchezo katamsaidia kujenga tabia ya kunywa maji. Unaweza pia kujaribu kukamua limao ama chungwa na kuongeza kidogo katika maji unayompatia mtoto.


Tumia kikombe maalum. Wakati binti yangu alikuwa na umri wa miaka miwili alipenda sana umalkia. Hivyo kuendana na matakwa yake tulimtafutia kikombe cha plastiki chenye mahadhi ya kimalkia-malkia na kumshawishi kukinywea 'maji ya malkia.' Mara zote alipenda mbwembwe hizi hivyo ilimwia vigumu kukataa kuyanywa 'maji ya malkia.' Zoezi hili bado linafanya kazi ingawa ameshakuwa mkubwa kiasi. Waruhusu watoto kuchagua kikombe maalum cha kunywea maji iwapo inawezekana. Kadiri wanavyoona 'umilikishwaji' katika zoezi zima ndivyo mafanikio yako katika unywaji wa maji utakavyoongezeka. Ungana nao katika zoezi hili, yaani uongoze kwa vitendo. Ukitoka kazini washawishi nyote mnywe maji, fanya hivyo pia kila baada ya chakula.


Wape uhuru wao. Watoto wadogo mara tu wanapohisi 'kujitegemea' hutaka uhuru kufanya 'watakavyo'. Katika ulaji, uvaaji na hata unywaji, nk. mtoto anataka afanye mwenyewe. Mtafutie glasi ama kikombe anachoweza kunywa maji bila ya msaada wako pasi na madhara. Usimwache kunywa maji katika glasi ya udongo iwapo bado hawezi kuishika pasi ajali pekee yake.


Zoezi la kunywa maji kama mazoezi mengine katika malezi huhitaji subira. Malezi ya watoto kwa ujumla wake ni kazi ya masaa 24 kwa siku miaka yake yote hadi atakapotimiza utu-uzima. Hivyo tunakutia moyo mzazi mwenzetu, shughuli hii bahati mbaya unajifunza kwa 'mafunzo-kazini'. Hakuna mahala katika ukuaji wako na utafutaji elimu / pesa wako uliandaliwa mahususi kwa ajili ya kuingia katika biashara ya uzazi hasa malezi ya watoto. Sote tupo darasani tukijifunza. Yataka moyo.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

0 views

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page