Mjadala wa mimba za utotoni na fursa ya kuendelea na masomo kwa watoto hawa bado unaendelea. Yafuatayo ni mambo yatakayosaidia kumuongoza binti yako kuepuka kujiingiza katika ngono akiwa na umri mdogo.
Mwambie mwanao wa kike kuwa unampenda na mkumbatie kwa upendo mara kwa mara. Inashauriwa jambo hili alifanye mzazi wa kiume mara nyingi ili mtoto azoee kulipokea kutoka kwa jinsia ya kiume. Mtoto pia hatozuzuliwa na mapenzi toka kwa mwanaume baki.
Mwambie mwanao ni mrembo kila mara, wazazi wote wanashauriwa kuzungumza na mtoto wao wa kike na kumsifia juu ya urembo wake lakini baba akitekeleza jukumu hili inakuwa inamjenga zaidi mtoto juu ya kujitambua na kutosumbuliwa aambiwapo hivyo na mwanaume anaemtaka kingono. Mfundishe jinsi ya kujibu aambiwapo hivyo, msifie kwa kumwambia ana macho mazuri, umbo zuri, mpe sifa zote wazitumiazo wanaume kuwarubuni watoto wa kike.
Mfunze mwanao kuridhika na hali halisi ya uchumi wa familia. Fanya mazungumzo na mwanao wa kike juu ya hali halisi ya maisha hapo nyumbani ili umuweke bayana juu ya kipato cha familia. Mnapataje fedha? Mnazitumia katika vipaumbele vipi?
Mwandae kuridhika na anachopewa nyumbani na kuepuka 'hongo' ndogondogo kwani tafiti zimeonesha vijizawadi kama pipi, mafuta ya kupakaa na manukato, soda na hata miwa hutumiwa na wanaume kuwarubuni mabinti hasa wanapokuwa shuleni.
Wazazi (hasa mama), mueleze bayana mtoto wa kike kuwa madhara mengi yatokanayo na tendo la ngono ni mzigo kwake kubeba. Atambue kuwa kubeba mimba ni rehani hasa katika umri mdogo. Kwamba kuna kufa au kupona katika miezi tisa ya ujauzito hasa kwa watoto. Kwamba yapo magonjwa ambata ya kila aina. Atambue namna ilivyo aibu kwa familia na unyanyapaa atakaoupata kuanzia ngazi anapotoka hadi aingiapo.
Pia mueleze bayana kuwa ngono na mimba hazitouacha mwili wake salama kimwili, kiakili na kama anamwamini Mungu, kiimani anakuwa katenda dhambi.
Elimu ya afya ya uzazi isiachwe nyuma. Wazazi tuache dhana ya kwamba kuongea na mtoto masuala ya uzazi ni aibu. Zungumza juu ya mabadiliko ya kimwili na maumbile. Mbona chuchu zinatokea? Ajue mimba inapatikana kwa kujamiiana 'athari za ngono' kama gonjwa na ukimwi na mambo mengine namna hii. Mueleze jinsi ya kuepuka 'mihemko' ya kibaolojia inayomsukuma kuwaza ngono. Kwamba anaweza kutumia muda huo kufanya mazoezi au kulima bustani ya mboga, nk. na kujishughulisha na mambo ya msingi kwa maendeleo yake.
Mfunze mwanao kutokuamini watu kirahisi hasa wanaume, awe ndugu, rafiki ama vinginevyo. Imani iwe na akiba ya mashaka. Mapema binti yako ajue linapokuja suala la ngono, ndugu wa karibu katika familia tandaa na rafiki wa familia wako mstari wa mbele kama 'waharibifu'. Jenga mawasiliano na mahusiano ya karibu na binti yako ili upate fursa ya 'kuhadithiwa' njama za 'wanaomnyemelea' kingono. Kama hakuna ukaribu, ujenge. Vipi akushirikishe katika changamoto anazokutana nazo za vishawishi vya kingono?
Watoto wa kiume wasiachwe nyuma. Wafundishe wavulana kuthamini utu na maisha ya dada zao na watoto wenzao wa kike kwa ujumla. Wafunze kuuthamini mchango wa mama zao katika maisha yao na jamii kwa ujumla. Wazazi wa kiume tuwe taswira kwa watoto wetu wa kiume kwa kuwaheshimu mama, dada, shangazi na watoto wetu wa kike kwa kuwapatia mapenzi na fursa sawa ndani ya familia. Akina baba tuache ngono na watoto wakike huku tukibainisha namna gani tungependa kuwalinda na kuwasaidia kuzifikia ndoto zao pale tunapozungumza na watoto wa kiume.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
Comments