top of page
  • C-Sema Team

Namna ya kumsaidia mama mjamzito akiwa kwenye uchungu wa uzazi.

Msaada mkubwa zaidi ambao unaweza kumpa mama mjamzito ajifungue kwa usalama ni kumtia moyo kwa upendo. Epuka kuingiza vidole vyako ukeni kuchunguza mlango wa kizazi. Hakuna ulazima wa kufanya hivyo katika hali ya uchungu wa uzazi wa kawaida. Hii inaweza kusababisha maambukizi kwa mama na mtoto. Usiminye au kubonyeza tumbo la mama au kutumia nguo au kitambaa kumvuta mtoto nje.Mara nyingi inashauriwa usiingilie kati kwa kujaribu kutatua lolote pale mama anapokuwa katika hali ya uchungu. Kufanya hivyo kunamuweka mama na mtoto salama.

Wakati wa mwanzo wa uchungu wa uzazi, mkunga na watu waliopo jirani mnapaswa kumtia moyo mjamzito. Mkumbusheni:

  • Kupumua pole pole, kupuliza au kuhema, au kuachia sauti zozote zile kupunguza maumivu wakati misuli inabana na kuachia.

  • Kunywa kidogo kidogo vinywaji laini kila baada ya muda mfupi, na kula kiasi kidogo cha chakula.

  • Kukojoa mara kwa mara. Kibofu kilichojaa mkojo huchelewesha kujifungua.

Muda wa uchungu wa uzazi. Kila mjamzito ana uchungu wa uzazi tofauti na hii ni kawaida. Uchungu wa uzazi unaweza kuwa wa haraka sana au kuchukua muda mrefu. Hata hivyo, baadhi ya watoto hukwama na hawawezi kuzaliwa bila matibabu au operesheni. Jipange kujua itachukua muda kiasi gani kufika hospitali. Iwapo unaishi mbali na hospitali basi anza mapema safari yako kuelekea hospitali.


Kusukuma mtoto. Mara mama mjamzito anapohisi haja ya kusukuma, anaweza kufanya hivyo kwa usalama. Mara nyingi wanawake hujua jinsi ya kusukuma wakati wa kujifungua bila msaada. Kamwe, usimkaripie mama mjamzito.


Kuchuchumaa, kupiga magoti huku umeegemea mikono au kupanua miguu huku umeegemea mito / kusheni mgongoni - yote ni mikao mizuri ya kusukuma mtoto. Kama mkao mmoja hauwezi kumtoa mtoto nje, jaribu mkao mwingine.

Hatua ya kusukuma mtoto kawaida huonekana kuwa nafuu kwa mama kuliko hatua za awali katika uchungu. Kama uchungu wa uzazi umechukua muda mrefu mama anaweza hata kusingizia kidogo na kila akishtuka anaendelea tena kusukuma.

Iwapo zoezi hili la usukumaji litakuchukua muda mrefu:

  • Mtie moyo mama abadilishe mkao.

  • Mwambie mama akakojoe. Kibofu kilichojaa mkojo hupunguza kasi ya uchungu.

  • Mruhusu apumzike katikakati ya zoezi hili halafu avute pumzi nzito ndani na kusukuma tena kwa nguvu kadri awezavyo.

Baada ya saa 2 za kusukuma kwa nguvu bila mafanikio tafadhali tafuta msaada wa daktari. Huenda operesheni ikahitajika kumtoa mtoto.

Zoezi la kujifungua linahitaji utaalamu wa kitabibu na uzoefu. Kamwe usijaribu kutumia maandiko haya kama elimu ya kutosha kuweza kujifungua nyumbani. Bado yapo mambo mengi katika zoezi la kujifungua yanayohitaji msaada wa mkunga au daktari. Nenda kajifungue hospitali kuepusha shari.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, Instagram @sematanzania na www.sematanzania.org


Picha ya makala haya ni kwa hisani ya WHO.

1 view

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page