top of page
C-Sema Team

Namna bora ya kumlea mtoto wa pekee kwenye familia

Katika makala haya tunaangalia namna ya kumsadia mtoto aliyezaliwa pekee kwenye familia ili kuondokana na madhara yatokanayo na malezi ya upweke. Ingawa ni nadra kuona familia zenye mtoto mmoja katika jamii zetu, zipo familia chache zilizo na mtoto mmoja tu. Baadhi ya familia huamua kuwa na mtoto mmoja kwa sababu mbalimbali zikiwemo sababu za kiafya (matatizo ya uzazi), kiuchumi, na kadhalika.


Namna bora ya kumlea mtoto wa pekee kwenye familia

Tafiti za kisayansi zinaonesha kuwa watoto wanaozaliwa pekee yao kwenye familia hudekezwa sana na wazazi wao kwa hofu ya kuwapotezea furaha (kuwaudhi), kama anavyoeleza Dk. Bernice Storensen mtaalamu wa saikologia ya malezi, katika baadhi ya maandiko yake. Wazazi hawapendi mtoto wao akose furaha kwa hiyo humpatia mara moja kile anachokihitaji, hata kama kina madhara kwa mtoto. Namna hii mtoto huharibikiwa katika mwenendo wa maisha yake. Watoto wa namna hii hupatwa na madhara mengine kama tunavyoainisha hapa chini.


Kupoteza uaminifu kwa watu wengine. Unapomlinda sana unamfanya asiwe na uaminifu katika kukua kwake akidhani hakuna mtu mwingine anayeweza kumpenda isipokuwa wazazi wake. Hii husababisha mtoto ashindwe kujenga marafiki na kuthamini watu wengine, hivyo kupata wakati mgumu kukabiliana na changamoto za jamii, pamoja na kushirikiana na wenzie.


Kumjengea dhana ya utegemezi. Watoto hawa hushindwa kujisimamia katika majukumu mbalimbali kwani kila linalowakabili wazazi wanalitatua na hivyo kuwa wavivu kufikiri, kukosa, ubunifu na udadisi wa mambo kwani muda mwingi matatizo yao hutatuliwa na wazazi.


Ubinafsi na uchoyo. Watoto hawa hawapendi kushirikiana na wenzao kwa vile vitu ambavyo wanavimiliki hawatopenda wengine waviguse kwa sababu katika kukua kwao kila kilicho mzunguka huwa ni chake, hivyo wamezoea kula, kunywa na kucheza peke yao.


Kujengewa uoga. Hii ni kwa sababu muda wote kwenye maisha yao wamekuwa na watu wachache waliowazunguka nyumbani. Tabia hiyo hujijenga na kumuathiri hadi anapoanza shule akashindwa kuchanganyika na watoto wapya kwenye mazingira yanayowazunguka.

Ili kumsaidia mtoto kuepukana na madhara haya, mzazi anatakiwa kumfunza mtoto kuishi kwenye jamii kwa kumjengea mazingira ya kucheza na kushirikiana na wenzake. Mtoto azoeshwe kuchanganyika na wenzake na atambulishwe kwa ndugu wengine wa familia kama vile shangazi, mjomba, baba wadogo, binamu n.k. ili kuweza kushiriakiana na kujifunza ujuzi kutoka kwa wenzake. Mpatie mtoto nafasi ya kuelewa kwamba alichonacho hata kama ni kidogo anaweza kugawana au kukitumia na walio mzunguka.


Mzazi hatakiwi kumlinda mtoto kupitiliza, mtoto apewe uhuru wa kucheza na kufanya mambo yake mwenyewe. Jukumu la mzazi libaki kumwongoza mtoto lakini si kumbana na kumzuia/kumfanyia kila anachokifanya.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

2 views
bottom of page