Tunapozungumzia malezi ya mtoto tunaangazia hatua zote za ukuaji wa mtoto tangu mimba inapotungwa hadi kipindi cha utoto kuisha. Kipindi cha utoto hutofautiana kutoka nchi na nchi; kwa hapa kwetu Tanzania, ni yule aliye chini ya umri wa miaka 18. Kila hatua ya ukuaji ina mahitaji yake na uangalizi maalumu toka kwa mzazi au mlezi.
Kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea kukua kwa kasi, imekuwa ni changamoto kwa wazazi kutimiza majukumu yao ya malezi ipasavyo. Mabadiliko haya yameleta tofauti kubwa katika maisha ya watoto katika hatua zote za ukuaji, hasa katika mazingira na vifaa ambavyo watoto wamekuwa wakitumia kuchezea. Wasiwasi umetanda kwa wazazi juu ya matatizo ya afya ya mwili kwa watoto yatokanayo na vyakula vya kisasa, madhara ya afya ya akili yatokanayo na matumizi ya vifaa vya kielektroniki, midoli na utazamaji wa vikaragosi (cartoons) pamoja na video zenye jumbe hatarishi kwa makuzi ya watoto.
Kabla ya teknolojia kuleta mabadiliko hasa ya wavuti (Internet) na matumizi ya mtandao, watoto wengi walikuwa wana muda wa kutosha kucheza nje ya nyumba na kujifunza mengi juu ya asili na halisi ya dunia inayowazunguka. Walicheza michezo ya kuwajenga kiafya na kuchangamsha akili kama kukimbia, kuruka na kucheza mpira na ile ya kuwajenga kiakili na kiubunifu kama vile kutengeneza vifaa mbalimbali kwa kutumia udongo, matope, miti, vitambaa vya nguo, kamba, mifuko, karatasi, sponji na vingine kadha wa kadha vilivokuwa vikiwazunguka katika mazingira yao.
Kutokana na hali hii, wazazi hasa wa mijini, wamekuwa wakipata changamoto ya namna gani watafanikisha uwiano kati athari za kiteknolojia na malezi bora kwa watoto. Kuna baadhi wanafikiri kumpatia mtoto vifaa vya kielektroniki vya kuchezea au kuwaacha waangalie televisheni muda wote wanaotaka ni jambo la kawaida na ni kutimiza wajibu. Kwakuwa mara nyingi watoto hufurahia sana vitu hivi kiasi cha kuwafanya watulie na hata waache kulia, kuuliza maswali na kuzunguka nyumba nzima, wazazi hutumia fursa hii kama namna ya kuwatuliza na kuendelea na shughuli zao.
Tafiti iliyofanywa hivi karibuni na madaktari wa watoto nchini Marekani inaonesha kuwa, watoto wa chini ya umri wa miezi 18 hawapaswi kutumia vifaa vyovyote vya kielektroniki; watoto wa chini ya miezi 18 hadi 24 wanapaswa kutumia vifaa hivyo kwa kutizama video au michezo yenye dhima za kuelimisha na dhima hizo zipitiwe na wazazi pia. Miaka 2 hadi 5 wanatakiwa kutumia muda wa saa moja tu kwa siku kutizama luninga au vifaa vingine. Miaka 6 inabidi wasimamiwe na waongozwe kwa ukaribu zaidi juu ya muda wanaoutumia kwenye vifaa vya kielektroniki.
Wazazi wanatakiwa kuwa makini kuhakikisha matumizi ya vifaa vya kielektroniki visiingilie na kuvuruga ratiba ya watoto ya kulala, kupumzika, kucheza, kuhusiana na marafiki, familia pamoja na kujisomea. Kama wazazi, tusibebwe na hisia za mabadiliko ya kiteknolojia tukidhani kuwapatia watoto vifaa vya kielektroniki ndio mapenzi kwa watoto wetu. Ukweli ni kwamba hata watu maarufu duniani tunaowaona wakitumia mtandao, wana taratibu za kudhibiti matumizi ya mtandao yaliyopitiliza kwa watoto wao. Jarida la US Magazine linatutaarifu kuwa familia za watu maarufu kama ya mtoto wa mfalme wa ulaya Prince William, Kourtney Kardashian, Jennifer Lopez na wengine wengi huwapa watoto wao dakika 30 tu za kuangalia video na michezo kwenye vifaa vya kielektroniki katika siku za wiki na dakika 60 tu katika siku za mwisho wa wiki huku wakitumia muda mwingi kucheza, kufurahi na marafiki, wazazi na familia pamoja na kujisomea.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
Comments