Katika makuzi kuna mambo yanayoweza kusaidia kuchangamsha akili ya mtoto na kumfanya afikirie na kuchanganua mambo au kumfanya awe na upeo mkubwa. Mtaalamu wa makuzi Gaye Gronlund anasema kuwa watoto wadogo hujifunza zaidi kwa kutumia michezo kwa kuwa michezo hujenga ubongo wa mtoto na kuimarisha uwezo wake wa kufikiria na kuchanganua mambo. Kuna michezo ambayo Gronlund ameainisha kuwa ni muhimu zaidi katika kuchochea ukuaji wa ubongo hasa kwa watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 8.
Watoto hupenda kuigiza wanapika. Iwe kwenye vigae, vibati ama kwenye vyombo vya kuchezea vidogo kama vinavyotumika nyumbani katika mapishi. Mara nyingi watoto huwaangalia mama zao wakipika chakula na baadae huigiza kupika. Hii huonekana kama wanacheza na kujifurahisha ila kuna cha ziada kinachofanyika kwenye ubongo. Mtoto anaanza kujenga uwezo wa kufuata hatua za mapishi kama vile kuigiza kusoma kunavyomfanya ajenge uwezo wa kuelewa kusoma.
Mchezo wa kujificha au kwa jina maarufu kombolela humjengea mtoto uwezo wa kudadisi mambo, uwezo wa kujua ramani na kutokukata tamaa pale mambo yanapokuwa magumu. Kwa mtoto mdogo asieweza kujificha mnaweza kubadili mchezo kidogo na kuficha kitu badala ya wewe au mtoto kujificha. Hakikisha unaficha kitu mahali ambapo unajua mwanao ana uwezo wa kukipata halafu mwambie akitafute. Akikipata atafurahi na pia utakuwa unamjengea uwezo wa kukisia mambo.
Michezo ya kujenga nyumba au muundo wowote kwa kutumia vitofali (bricks) ni ya muhimu sana kwa mtoto na humjengea uwezo wa uvumbuzi. Hii michezo humfanya afikirie, Je, nikiweka tofali hili juu ya hili nini kitatokea? Na je nijenge nini? Atafikiri na kuweza kufanya maamuzi sahihi na kutambua kama amekosea au la! Hii itampa chachu ya kufikiria zaidi.
Watoto wanajifunza zaidi tukiwafuata na sio wao wakitufuata. Hivyo ni vyema kumuacha mtoto aongoze mchezo pale mnapokua mnacheza wote na wewe ufuate anachokifanya. Mathalani akichimba shimo kwenye mchanga usimsaidie kuchimba bali fuata mfano wake na kumuuliza maswali elekezi pale unapoona anapata shida. Kwa kujibu maswali haya, mtoto atapata uvumbuzi pale alipokuwa amekwama.
Michezo mingine ni kama kujaza mchaga au maji kwenye vikopo kwa kutumia vijiko vidogo. Michezo kama hii mnaweza kucheza kwenye fukwe za bahari au maziwa au kwenye mchanga mlaini. Katika muda huu, jaribu kuwa makini na mtoto kumjengea uwezo wa kujua ulimwengu unaomzunguka. Tumia fursa hii kuuliza maswali yenye majibu ya kujieleza (open ended question). Mtoto kamwe hatosahau muda huo.
Kuvaa nguo mwenyewe inaweza kuwa kama mchezo kwa mwanao. Kuna dhana imejengeka kuwa watoto ni lazima wachaguliwe nguo kutokana na mzazi anavyojisikia na pia kuvalishwa. Hii sio sahihi, Gronlund anashauri mtoto anapofikia umri fulani apewe nafasi ya kuvaa mwenyewe na kuchagua rangi atakazo. Sio lazima kila siku lakini mara moja moja umpe uhuru huu. Anajenga uwezo wa kufanya maamuzi sahihi na wa kujifanyia mambo mwenyewe.
Baadhi ya watu huona michezo hii ya watoto kama michezo ya kawaida tu ila ina manufaa kadha wa kadha katika kuweka motisha kwenye makuzi ya ubongo ambayo ni muhimu kwa Siku zote mzazi usimkataze mtoto kucheza, kama hautaki achafue mazingira, muonyeshe sehemu na njia sahihi ya kuchezea huo mchezo wake.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
Comments