top of page
  • faithmkony

Malezi ni chachu ya utu.

   

      

Malezi ni mchakato wa kumtunza, kumuelekeza, kumuongoza na kumuelimisha mtoto tangu angali tumboni hadi anapofikia umri wa kujisimamia mwenyewe. Mchakato huu unahusisha kuhakikisha mahitaji ya mtoto yanakidhiwa,kumfundisha stadi za kazi na maarifa muhimu yatakayosaidia kujenga na kukuza uhusiano mzuri na wanao mzunguka kuaznia ngazi ya famili, shuleni na kwenye jamii.

 

Malezi ni kipande muhimu sana katika maisha ya mtoto.Kila mtoto anahitaji malezi bora ili kuwa na maendeleo kamili ya kiakili, kihisia, na kijamii, kiuchumi na kiroho. Malelzi sahihi huzaa matunda mazuri, yakimsaidia mtoto kuwa na utu na kuwa raia mwenye maadili mema. Katika jamii zetu, malezi yamekuwa msingi wa kukuza vijana wenye mchango kwa taifa na wale ambao wameharibikiwa. Malezi ni zaidi ya kumpa mtoto shibe na makaripio, ni mchakato unaohitaji kujitolea, upendo, huruma, uvumilivu na uelewa wa kina juu ya mahitaji ya maendeleo na makuzi ya mtoto.

 

Malezi chanya unayompa mtoto angali mdogo ndiyo chanzo cha utu wake wa kesho anapo kuwa mtu mzima, hii inamaanisha kwamba kama mzazi au mlezi atakuwa anamlea mtoto katika mazingira ya kikatili inamasnisha hata mtoto atakapokuwa mkubwa atakuwa katili au atakuwa na tabia za kikatilii kwasababu ya Malezi aliyoyapata alipokuwa mdogo. Hivyo hivyo mtoto atakapolelelewa katika malezi yaliyobora na mazuri, yenye upendo, kujali, kusikilizwa, kupewa nafasi ya kucheza, kuwa na mazingira yenye amani na utulivu katika familia na jamii kwa ujumla atakuwa na tabia njema na nzuri atakapokuwa mkubwa.

 

Kwahiyo malezi ya utotoni yana athari kubwa (hasi na chanya) kwa mtoto atakapokuwa mkubwa. Hivyo basi inashauriwa wazazi kuwa makini katika njia au mbinu tunazotumia kulea watoto wetu.

 

Kila mtoto ni wa kipekee, na malezi yanahitaji kuwa yanaendana na mahitaji ya mtoto binafsi. Hii inamaanisha kuwa mzazi au mlezi tunahitaji kuelewa tabia, umri, mazingira, mapendeleo, na mahitaji ya mtoto ili kumsaidia kufikia uwezo wake wa juu. Kwa mfano, mtoto ambaye ni mtukutu anahitaji sana ukaribu, uvumilivu, kuelekezwa bila kukata tamaa na kuzungumza nae mara kwa mara, mtoto mpole na msikivu anahitaji uangalizi wa karibu na kuongozwa bila kutumia nguvu nyingi.

 

Zifuatazo ni sababu zinazoelezea kwanini malezi ya mtoto ni chachu ya utu

 

Chanzo cha nidhamu. Malezi ni chanzo cha nidhamu ya mtoto na ndo maana kuna methali inayosema kwamba mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Inamaanisha nidhamu atakayofunzwa na wazazi, mtoto atakaua nayo mpaka atakapokuwa mkubwa na huo ndio utakao kuwa utu wake. Hivyo basi, ikitokea mzazi amefeli katika nidhamu wakati mtoto akiwa mdogo hivyo ndivyo mtoto anapokuwa ameharibikiwa utu wake.

 

 

Malezi humsaidia mtoto kutengeneza mahusiano mazuri na watu katika jamii. Malezi bora yanayopatikana nyumbani na shuleni humsaidia mtoto kujenga mahusiano ya karibu na watu sahihi katika jamii. Katika jamii ya Tanzania, mfano mzuri ni jinsi wazazi wanavyowafundisha watoto kuhusu heshima na adabu, ambayo ni muhimu kwa mahusiano ya kijamii. Kwa mfano, mtoto anayepokea malezi ya kutambua na kuthamini umri na uzoefu wa watu wa familia na majirani, hujifunza kuwa na mawasiliano mazuri na watu mbalimbali. Aidha, kushiriki katika klabu za michezo na vikundi vya kidini vinavyohusisha watoto na vijana husaidia kuwajengea maadili na ushirikiano na jamii yao.

 

Malezi humsaidia mtoto kufanya maamuzi sahihi. Malezi mazuri yanamsaidia mtoto kufanya maamuzi sahihi katika maisha yake. Katika jamii ya Tanzania, wazazi na walimu wanatoa maelekezo kuhusu maadili na mbinu za kutatua migogoro ili mtoto aweze kufanya maamuzi bora. Kwa mfano, mtoto anayeelezwa kuhusu umuhimu wa elimu na jinsi ya kuchagua njia sahihi za masomo na marafiki sahihi anakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kuhusu masomo, taaluma na tabia kwa ujumla. Vile vile, malezi yanayojumuisha kujenga tabia za uwajibikaji na mipango, kama vile mipango ya familia kwa watoto wanaokua, husaidia watoto kuamua kwa umakini kuhusu mambo kama vile ajira, mahusiano na matumizi ya fedha. Hivyo, malezi bora hutoa mwongozo muhimu kwa watoto katika kufanya maamuzi yenye tija kwa maisha yao.

 

Malezi mazuri ni mfano mzuri kwa mtoto. Watoto hujifunza na kuangalia kila kitu kutoka kwa wazazi wao na kisha kufanya kitu kilekile mzazi alichofanya. Hivyo, kama mzazi ana malezi mazuri, anawajibika kwa watoto wake na ana upendo kwa familia yake inamaanisha kuwa mtoto pia ataiga kile anachokifanya mzazi na kuja kufanya katika familia yake ya badae na hivyo kuendeleza kizazi cha watu wenye utu kwenye jamii.

 

Malezi mazuri ni chanzo cha tabia njema. Watoto wanahitaji kusikilizwa, kuelekezwa na kushauriwa. Pale mtoto anapokosea anahitaji kuelekezwa ili kufanya kitu sahihi. Pia, mtoto anapojiingiza kwenye tabia mbaya mzazi anatakiwa kumuelekeza na kama inawezekana kumuadhibu kwa njia yenye kumfunza na si kumuumiza ili aweze kutokomeza tabia mbaya na kuimarisha tabia nzuri na kujenga utu ndani yake.

 

Wazazi na walezi inabidi tutambue kwamba tabia njema au mbaya huanzia nyumbani kutokana na malezi aliyopewa na mazingira aliyokuzwa mtoto.

 

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org (http://www.sematanzania.org/ )

1 view

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page