top of page
  • C-Sema Team

Maandalizi ya watoto kurudi shuleni

Likizo zimekwisha na shule nyingi hasa zile za uma zinaanza muhula wa masomo juma hili. Tumekukusanyia dokezo chache toka kwa wazazi waandamizi, wengi sasa wastaafu - hii hapa ni orodha iliyoandaliwa kutokana na uzoefu wao.


Maandalizi ya watoto kurudi shule

Mie huwa nalipa ada Oktober na Novemba kuepusha madhara ya Disemba na Januari.

Lipa ada ya shule ya mtoto wako Oktoba au Novemba ili kuepuka athari za Januari. Wazazi wengi huuona mwezi wa Januari mchungu mno kwani ada za shule huwakabili msimu huu. Tulivyozungumza na mtaalamu na Mkufunzi Mwandamizi wa Sheria Dk. Mashamba, tulibaini kwamba yeye hulipa ada za shule mwezi wa Oktoba au Novemba na si Januari ili kuepuka madhara yanayotukumba wengi wetu sasa. Huwa nalipa kidogo kidogo. Bahati nzuri nimekuwa nikilipa ada ya dependants wangu since 1999, hivyo nimeshakuwa mwandamizi wa kulipa kidogo kidogo, sisubiri hadi Januari, alimalizia Dk Mashamba.


Anza ratiba ya kulala mapema wiki moja kabla ya shule ili mtoto wako apate angalau saa 10 za usingizi usiku.

Hata sisi watu wazima tunajua jinsi tunavyopata wakati mgumu kuamka tunapochoka, iweje rahisi kwa watoto wetu? Kumbuka kwamba hawana ujuzi tulionao wala sababu tulizonazo kukabiliana na uchovu wa kudamka mapema, tuwape fursa kujiandaa.


Zungumza

Zungumza na watoto wako kuhusu hisia zao na wape nafasi ya kushiriki katika mazungumzo ya wazi huku ukifanya makusudi wa kudhibiti mjadala. Usiwaaibishe wala kuwavunja mioyo watoto wako. Waulize jinsi ambavyo wangependa kusaidiwa katika msimu huu wa maandalizi ya kurudi shule - mambo ambayo wazazi mnaweza kufanya na yale ambayo wazazi mnaweza kufanya kwa kushirikiana na watoto ili maandalizi ya kurudi shuleni yawe safi. Mfano kabla ya kutoka kwenda kufanya manunuzi ya mahitaji ya shule, ikitegemea umri na uelewa wa mtoto tengenezeni orodha ya vitu mnavyohitaji. Kubalianeni kulingana na uwezo wa fedha iliyopo kabla ya kwenda madukani. Kamwe usitoe ahadi za uongo kwa mtoto wako.


Je umezungumza na mwalimu wa mtoto / watoto wako likizo hii?

Kuwajulia hali na kumtakia heri ya mapumziko au mwaka mpya? Mazungumzo yawezakuwa kwa simu ama kwa kuonana. Vilevile yanaweza kuwa juu ya mada nyingine tofauti na salamu. Uzoefu tuliokusanya unaonyesha kuwa uhusiano mzuri kati ya wazazi na walimu umekuwa na matokeo mazuri katika elimu ya watoto wako. Ifanye tabia kuzungumza na mwalimu wakati wote hata likizo. Unapozungumza na mwalimu muonyeshe kujali ustawi wa mtoto wako na utu juu ya kazi njema anayoifanya. Mwambie dukuduku lolote ulilonalo juu ya maendeleo ya watoto wako - namna hii mtatatua kwa pamoja kama timu.


Maandalizi

Maandalizi madogo-madogo kabla ya siku ya kufungua shule yanaweza kuwapa nyote wepesi wa mtoto wako kurudi shuleni. Watoto wadogo kabisa wakumbushe umuhimu wa kwenda shule kwani mara nyingine hawajui kwa nini waende? Waeleze hili kwa upendo wa dhati. Huwezi kuwaharibu watoto wako kwa upendo.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

0 views

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page