top of page
  • C-Sema Team

Kwanini mzazi unahitaji elimu ya huduma ya kwanza kwa mtoto wako

Watoto wawapo nyumbani hujihusisha na michezo mbalimbali ambayo kwayo huburudishwa na kuwajengea mahusiano bora. Kila hatua ya ukuaji wa mtoto huambatana na matukio kadha wa kadha yenye kufurahisha, ingawa pia wakati mwingine matukio hayo hayo huweza kuhatarisha maisha na usalama wa mtoto awapo nyumbani au katika mazingira mengine.


Swali la kujiuliza ni je, wazazi tuna uelewa gani kuhusu elimu ya huduma ya kwanza kwa mtoto pindi inapotokea dharura katika nyumba zetu?


Utakubaliana nasi kuwa wazazi tulio wengi hatuna uelewa wa kutosha juu ya elimu ya huduma ya kwanza kwa watoto wetu, na hivyo inapotokea dharura katika nyumba zetu au maeneo mengine sisi huishia kutapatapa pasipo kujua tufanye nini ili kuokoa hali ya hatari inayomkabili mtoto.

Wiki chache zilizopita katika basi la abiria aliketi mama na mtoto mdogo (umri miaka miwili au mitatu). Yule mtoto alikua akilia sana labda sababu basi lilikua kwenye foleni na hali ya hewa ilikua nzito sana mle garini. Dakika chache baadae ghafla mtoto akaacha kulia. Kumbe mtoto alikuwa hapumui tena. Kwa haraka sana yule mama akashuka kwenye basi huku akipiga mayowe na kilio. Alichanganyikiwa. Abiria wote walipigwa butwaa. Makelele na minong'ono ilitawala.


Bahati nzuri akatokea mama mmoja aliemchukua mtoto kumlaza chali na kuita jina la mtoto karibu na sikio lake, pia alimsaidia kumpa hewa kwa njia ya mdomo kwa mdomo (kati yake na mtoto). Mtoto alizinduka na hivyo kukimbizwa hospitalini na mama yake.

Kisa hiki kinadhihirisha umuhimu huduma ya kwanza (First Aid). Huduma hii ni msaada unaotolewa kwa mtu anayekabiliwa na ugonjwa au madhara ya ghafla pindi ambapo daktari hayupo karibu au kabla hajapelekwa hospitali kwa matibabu zaidi.


Kimsingi yapo baadhi ya matatizo ambayo huweza kumalizwa kwa huduma ya kwanza. Mfano kama mtoto wako anapopatwa na maumivu au homa ya muda mfupi, majeraha madogo, kushtuka mguu au mkono n.k. Hata hivyo endapo tatizo litaendelea hata baada ya kutoa huduma ya kwanza ni muhimu kumkimbiza hospitali mara moja. Mzazi au mlezi unashauriwa kuweka kisanduku la humu ya kwanza ambacho kina zana muhimu kukusaidia kutoa huduma hiyo.


Kisanduku cha huduma ya kwanza pia huja na mwongozo wa jinsi ya kutumia vifaa vilivyomo katika kutoa huduma husika. Hujumuisha vifaa kama pamba, bendeji, spiriti,dawa za vidonge n.k. Mzazi au mlezi ni muhimu sana ukawa na kisanduku hiki nyumbani (na hata katika gari lako) kwani huko ni sehemu ambapo watoto huishi na kucheza michezo mbalimbali inayoambatana na hali ya hatari ambayo inaweza ikahitaji huduma ya kwanza.


Visanduku vya huduma ya kwanza hapa nchini hupatikana katika ofisi za shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross), maduka ya madawa na maduka ya vifaa vya ulinzi. Ipo haja sasa ya kupata kisanduku cha huduma ya kwanza kama sehemu ya tahadhari katika ulinzi wa mtoto wako.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

2 views

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page