Moja ya majukumu ya wazazi ni kulea na kuendeleza vipaji vya watoto wao. Dunia ya leo yenye ushindani mkubwa inahitaji maandalizi ya watoto wetu ili wawe katika nafasi nzuri kushindana. Upo uhitaji mkubwa wa kipaji cha mtu binafsi ukiachana na elimu anayopewa na sisi wazazi ndiyo wenye jukumu la awali kuibua, kupalilia na kukuza vipaji ndani ya watoto tuliojaaliwa.
Jenga ukaribu na mtoto. Utajiuliza naanzia wapi kuibua vipaji vya mtoto? Tenga muda kwa ajili ya kuwa karibu na mtoto mwangalie akicheza. Mjibu maswali yake kadiri unavyoweza. Kamwe usimdanganye mtoto ama kumpa jibu usilo hakika nalo. Mwambie hujui itamsaidia kuwa mkweli anakuwa hana hakika na jambo.
Zungumzeni. Kwa upekee kabisa utatambua mambo muhimu anayoyatilia mkazo mwanao. Namna hii utajua tu ametunukiwa vipaji katika maeneo gani. Msaidie kujenga matamanio na kukuza kipaji chake kwa kumtafutia hata vitabu, makala na majarida aendelee kujijenga katika eneo uliloona anaegemea.
Je ungependa arithi kazi / biashara yako. Wewe ni daktari, mwalimu ama mfanya-biashara na unapenda mtoto wako afuate nyayo zako. Mfano wa kuiga ni wafanya-biashara na Watanzania wenzetu wenye asili ya Asia, hasa wale wenye asili ya India, Bangladeshi na Pakistani. Wao huanza kwa kuwataka watoto wao watembelee biashara zao kila ipatikanapo nafasi. Mara nyingi jioni baada ya kurejea toka shule watoto huwepo kazini kwa wazazi wao kujifunza kazi ya mzazi na hata kusaidia kurudisha chenji kwa wateja.
Kwamba mwanao aje ofisi kwako mara moja moja kujifunza namna unavyofanya kazi. hata baadhi ya shule za msingi hapa Dar es salaam zinayo programu ya kuwapeleka watoto maofisini kwa wazazi wao ili wajue baba / mama zao wanavyofanya kazi / namna gani. Hii programu ni mfano mzuri katika kurithisha kazi ya baba / mama kwa mtoto.
Wekeza. Ifahamike pia kuwa wachezaji wengi wa soka na michezo mingine duniani walianza kujengwa wakiwa watoto. Serena Williams mchezaji maarufu wa tenesi aliandaliwa utotoni na baba yake. Romelu Lukaku Mbelgiji mwenye asili ya Congo na mchezaji wa klabu ya Machester United na timu ya taifa ya Ubelgiji alirithishwa soka na baba yake mzazi kwa kumsajili shule (academy) ya kukuza vipaji katika soka.
Mchezaji Cristiano Ronaldo wa klabu ya Juventusa maarufu nchini Italia baada ya kugundua kipaji cha mtoto wake katika soka alimsajilisha katika klabu ya watoto (shule - academy) walio chini ya umri wa miaka 9.
Hata Mmarekani mweusi maarufu daktari Ben Carson ambaye ni daktari bingwa wa upasuaji na Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Miji nchini humo yeye ni zao la juhudi binafsi za mama yake. Uwekezaji wa mama na ufuatiliaji wa karibu ulimpa mafanikia mwanae.
Mifano hii ipo mingi malezi ni kazi inayojumuisha ukuzaji vipaji na ipo zaidi juu yako mzazi / mlezi. Ni nadra sana mafanikio ya watoto kuja kwa bahati mbaya. Anza sasa kujenga ukaribu ili kujua matamanio ya mtoto wako. Ujue kajaaliwa kipaji kipi. Aje 'ofisini' kwako kumuandaa kurithi biashara ya familia na zaidi ya yote wekeza muda na rasilimali kumjenga.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
Picha ya makala ni kwa hisani ya gazeti la Mwananchi.