Marehemu alikuwa anasoma wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Kibeta iliyoko Manispaa ya Bukoba, jina lake ni Sperius Eradius amefariki akiwa na miaka 13, baada ya kipigwa na mwalimu wake akituhumiwa kuiba pochi ya mwalimu.
Siku ya tukio marehemu Sperius Eradius alikwenda kumpokea mizigo mwalimu wake aliyefika shuleni hapo kwa usafiri wa bodaboda, lakini baada ya mwalimu kuingia ofisini alianza kulalamika kutoiona pochi yake.
Mtoto huyu aliitwa na kuanza kuhojiwa kuhusu kupotea kwa pochi hiyo na akakana kuichukua, hali iliyosababisha kuanza kupigwa akitakiwa kuirejesha. Wanafunzi wenzake walihimizwa kuitafuta pochi hiyo mpaka chooni, lakini hawakuiona huku Sperius Eradius akiendelea kuadhibiwa.
Pochi ilipatikana. Cha kusikitisha ni kwamba wakati marehemu akiendelea kupigwa, dereva bodaboda alifika shuleni hapo akimtafuta mwalimu aliyepoteza pochi na kumkabidhi pochi aliyokuwa ameisahau kwenye pikipiki yake. Baada ya pochi hiyo kupatikana, mmoja wa walimu aliagiza Sperius Eradius apatiwe juisi na bagia, chakula ambacho hakuweza kukila kutokana na maumivu.
Kesi dhidi ya walimu hao (yaani aliyepoteza pochi na aliyetoa adhabu) imeendeshwa ndani ya siku thelathini na kutolewa hukumu na Jaji Lameck Mlacha. Mwalimu Heriet Gerald aliyeibiwa pochi ameachiwa na Mahakama Kuu. Wakati mwalimu Respicius Mtazangira akianguka kizimbani baada ya kuhukumiwa kifo kwa mauaji ya mwanafunzi.
Washtakiwa wote walishtakiwa kwa kosa la mauaji ya makusudi ya mwanafunzi Sperius Eradius. Katika hukumu iliyosomwa kwa saa mbili, Jaji Mlacha amesema upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha ushiriki wa Heriet kwenye kifo cha Sperius, huku Respicius akitiwa hatiani na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.
Kuhusu nia ya kuua, Jaji Mlacha amesema Mwalimu Respicius ambaye alikuwa akisimamia nidhamu, alimpiga kwa fimbo ya kawaida mwanafunzi huyo na baadaye kutumia kuni, jambo lililosababisha majeraha kwenye mwili wa mwanafunzi huyo na ni ushahidi kuwa alipigwa mara nyingi.
Ushahidi wa daktari. Mahakama imezingatia ushahidi wa daktari wa magonjwa na vifo kutoka Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza, Dr. Kahima Jackson ambaye alisema kifo kilisababishwa na mshtuko uliotokana na kipigo.
Tunapenda kuwakumbusha wazazi, wanafunzi, walimu, washika dau pamoja na wananchi wote kuwa mnamo mwaka 2002, Serikali ya JMT kupitia Wizara ya Elimu ilitoa Waraka wa Elimu (Na.24) Kuhusu Adhabu ya Viboko na kuweka utaratibu mahususi wa utolewaji wa adhabu ya viboko.
Adhabu hiyo inaweza kutolewa endapo kutatokea utovu wa nidhamu uliokithiri ama kwa makosa ya jinai yaliyotendeka ndani ama nje ya shule yenye muelekeo wa kuishushia shule heshima. Waraka huu pia unaongeza kuwa adhabu ya viboko itakayotolewa sharti izingatie ukubwa wa kosa, umri, jinsi na afya ya mtoto na isizidi viboko vinne kwa wakati mmoja.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
Picha: Mwananchi Communications.
Commentaires