top of page
  • C-Sema Team

Kwa nini mahusiano ya karibu na mtoto wako ni muhimu kwa ukuaji wake?

Mabadiliko ya mfumo wa maisha hasa katika utafutaji yamewafanya wazazi walio wengi hukosa muda wa kuwa karibu na watoto wao. Hivyo watoto wengi hasa sehemu za mijini wanashinda kutwa nzima na wasaidizi wa kazi za nyumabani ambao mara nyingine nao bado ni watoto. Ifahamike kuwa ili mtoto apate kurithi tabia zinazofanana na zile za wazazi / walezi wake inayumkinika lazima apate kuwa karibu nao. Awasikilize wanavyozungumza, ajifunze namna bora ya kuwasalimu wageni na mambo mengine mengi madogo madogo anayoyapata moja kwa moja kwa kukaa karibu na wazazi / walezi wake.


Twafahamu kuwa wazazi wengi hupenda kuwa walezi bora na siyo bora wazazi! Iwapo ni matamanio yako kuwa mlezi bora basi tukupendekezee kuwa namna bora ya kufanikiwa katika tamanio hili ni kwa kutumia muda wako katika kujenga na kukuza mahusiano ya karibu na mtoto wako. Ujue ameshindaje shuleni. Marafiki zake uwadadisi na ikiwezekana ifike mahala muwe marafiki kiasi cha yeye kukwambia mipango alonayo ya siku, wiki na hata ile ya muda mrefu.

Pata fursa ya kushawishi maono ya mtoto wako ya muda mrefu. Uhusiano wa karibu kati yako na mwanao hukupa nafasi ya kufanya nae mazungumzo, kucheza nae na hata kushuhudia yale mambo yote ya msingi ambayo mtoto wako huyapa uzito, na hivyo mapema unapata nafasi ya kushawishi aachane na mambo unayojua hapaswi kuyapa uzito. Taratibu unashiriki katika kujenga hulka yake na mwishowe tabia yake.


Mapenzi. Wataalamu wa malezi wanakubaliana kuwa hakuna mapenzi yalopitiliza kwa mtoto. Mtoto anahitaji kulelewa kwa upendo huku ukimjali ili kuwa na uwezo wa kujenga mahusiano salama na awe mweye kujali atakapokuwa mtu mzima. Kwamba mtoto anapogundua viashiria vya kupoteza au kuwa na hatari ya kupoteza ukaribu na wazazi wake huingiwa na hali ya mfadhaiko.


Mtoto ambaye amejenga ukaribu na wazazi wake huwa na msingi mzuri wa kujenga uaminifu katika mazingira yake na kwa wale wanaomzunguuka. Mwanasaikolojia maarufu John Bowlby anashauri kuwa kigezo muhimu sana katika kujenga ukaribu ni mgusano chanya ambao unaweza kupatikana kwa matendo kama vile kumbeba mtoto wako, kumtazama ana kwa ana, kutabasamu, kumbusu, kuimba na kucheka anye. Vyote hivi anasema John Bowlby husisimua kemikali katika ubongo ambazo huhusika katika kuufanya ubongo kujenga dhana ya ukaribu kati ya mtoto na mzazi wake.


Kujenga ukaribu kwa mtoto wako ni muhimu sana katika kipindi chote cha utoto wake hadi kufikia umri wa kujitegemea. Kukosa au kutojenga ukaribu wa kutosha huweza kusababisha matatizo katika maisha yote ya utoto hadi utu-uzima. Ndugu mzazi, ni muhimu kufanya jitihada za dhati za kumwendeleza na kumpenda mtoto kwa manufaa ya jamii na taifa. Wakati ni sasa!


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

0 views

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page