top of page
  • C-Sema Team

Kuelekea siku ya mtoto wa kike dunia: Tuongeze juhudi kupinga ukeketaji.

Ukeketaji wa wanawake ni utaratibu ambapo viungo vya siri vya wanawake hujeruhiwa au hubadilishwa. Jambo hili linaweza kuathiri sana afya ya wanawake na watoto wa kike katika maisha yao ya baadae. Wasichana wengine hufariki kutokana na kupoteza damu au kwa ugonjwa wa kuambukizwa kutokana na utaratibu huu.


Wanawake waliokeketwa wanaweza kupata matatizo wakati wa uzazi. kwa kawaida ukeketwaji hufanywa kwa wasichana wenye umri kati ya mwaka 1 na 15. Kunaweza kujulikana kama kutahiriwa kwa wanawake, kukata n.k. Kuna aina nyingi za ukeketaji kama vile kuondolewa kwa sehemu au jumla kwa kinembe / kisimi, kuondolewa kwa sehemu au jumla ya kisimi na midomo ya ndani ya uke (ni ile "midomo" inayozunguka uke), kutolewa kwa kupunguza au kukata kwa jumla kwa uke ikiwa ni pamoja na kisimi.


Aina hii ya ukeketaji hufanyika kwa kushona mwisho wa midomo ya uke na kuacha tundu dogo (kupunguza tundu). Aina ya mwisho ya ukeketaji ni kukata, kuchoma, kurarua, kutoboa na kutanua sehemu za siri za uke.


Baada ya kuzifahamu aina za ukeketaji sasa tuzungumze ni kwa nini ukeketwaji hufanywa? Kwa kawaida wazazi wa msichana au ndugu na jamaa zake hufanya mipango ili yeye akeketwe. Sababu za kukeketa ni pamoja na desturi za baadhi ya makabila, imani za kidini, njia za kuhifadhi bikira, wengine hufanya kwa ajili ya usafi, kulinda heshima ya familia. Lakini wengine hufanya ili kukubalika katika jamii haswa linapokuja suala zima la ndoa kwani wanaume walio wengi katika jamii za namna hii katu hawaoi wanawake wasio keketwa.


Ukeketwaji ni kinyume cha sheria za nchi ya Tanzania na hata mataifa mengi duniani. Ingawa ukeketaji ni kinyume cha sheria bado kosa hili hufanyika hapa kwetu Tanzania na inakadiriwa kwamba mwanamke 1 kati ya wanawake 10 mwenye umri kati ya miaka 15 - 49 alikeketwa. Kwa sasa ukeketaji hufanyika kwa kiwango kikubwa katika mikoa ya Manyara 58%, Dodoma 47%, Arusha 41%, Mara 32% na Singida 31%. TDHS MS 2015-2016.


Ingawa ukeketaji hufanyika zaidi vijijini baadhi ya makabila hufanya hata mijini. Wengi husingizia tarehe ya siku ya kuzaliwa (birth day) kumbe ni kumkeketa mtoto wao. Ukeketji unaleta madhara mengi kwa wasichana na wanawake ikiwa ni pamopja na maumivu yasiyokwisha sehemu za uke, magonjwa ya kuambukizwa ya mara kwa mara ambayo yanaweza kusababisha utasa (usiweze kuzaa), kutoka damu sehemu za uke, uvimbe na majipu sehemu za uke, matatizo wakati wa kukojoa au kuvuja na mwisho ni matatizo ya uzazi ambayo huweza kuleta kifo hasa wakati wa kujifungua kwa mama aliyekeketwa.


Ingawa juhudi za serikali ni nyingi katika kupambana na tatizo hili. Mwananchi na mzazi mmoja mmoja anayo nafasi ya kumlinda binti yake dhidi ya vitendo hivi. Ifikie mahala tuwape fursa mabinti zetu wasome pasi na kughasiwa na mambo namna hii. Kumnyima ukeketaji ni kuijali na kuithamnini afya ya mtoto wa kike. Hatujachelewa inaanza na wewe. Inaanza na mimi. Kamwe tusikae kimya hasa tunapojua kuwa mipango ya ukeketaji inapangwa. Mara moja tuwafahamishe jeshi la polisi ama idara ya ustawi wa jamii.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Instagram: @sematanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

0 views

Recent Posts

See All

Комментарии


bottom of page