top of page
  • Writer's pictureNadhira Jiddawi

Jinsia ya mtoto isiwe sababu ya kunyimwa malezi makini.

Katika makala haya tunaangazia uhusiano uliopo kati ya jinsia ya mtoto na malezi anayopatiwa na wazazi wake. Wapo wazazi ambao wangependa kuwa na mtoto wa kike na wengine wa kiume, ila wanapata watoto wa jinsia wasizotarajia.


Chaguzi ya kupata mtoto wa kike au wa kiume imekuwa ikiwatesa wazazi wengi kwa muda mrefu sana, hasa baada ya kupata mtoto tofauti na jinsia waliyoitarajia, yaani mzazi alipenda apate mtoto wa kike lakini akapata mtoto wa kiume, au wa kiume akapata wa kike.


Wazazi hawa baada ya kupata mtoto nje ya matarajio, wameishia kuwanyanyasa watoto hawa katika jamii tunazoishi. Tunashuhudia watoto wa kike au wa kiume wakitengwa na wazazi wao. Hii inatokana na mzazi tayari alishauandaa ubongo wake kwamba mtoto wa jinsia fulani ndio chaguo lake, hivyo inapotokea mtoto wa jinsia asiyoitarajia akakosekana, basi mzazi hupata shida kukubali kwamba alichokipata ndicho Mungu alichomjaalia.

Watoto hawa wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa namna mbalimbali kwa kuwa mzazi hakutarajia kuwa na mtoto wa jinsia ile aliyoipata. Kwa mfano ukatili wa kihisia. Hutokea pale mzazi anapomwambia mtoto nimekuzaa kwa bahati mbaya - kutengwa, kutukanwa, kutotimiziwa mahitaji yake ya msingi kwa sababu tu walichokipata hawakukitarajia. Watoto hawa hujikuta hawana upendo kutoka kwa mzazi mmoja au wote na tafiti zinaonyesha kuwa watoto namna hii huamua kuutafuta upendo nje ya familia zao na mara nyingi wanadanganywa na kufanyiwa ukatili zaidi.


Je, nini mzazi anatakiwa kufanya pale anapopata mtoto wa jinsia asiyotarajia? Kutokana na Utafiti wa kisayansi uliofanywa na Dr. Kathleen Moritz Rudasi kutoka Baraza la kitaifa la watoto wenye vipaji huko Marekani, mzazi ndiye kiungo muhimu katika kukuza matakwa, thamani, na ujuzi wa mtoto. Hivyo mzazi hatakiwi kuwaza kwamba mtoto wa kiume ni bora kuliko wa kike au wa kike ni bora kuliko wa kiume. Kwamba mzazi anatakiwa kufahamu kuwa chaguzi ya jinsia ya mtoto inafanywa katika pilika za kuutafuta ujauzito na si wakati wa kujifungua. Kwamba chini ya ushauri wa daktari ndipo mke na mume wanaweza kupanga jinsia ya mtoto wanayemtaka.


Pia mzazi anashauriwa kuuandaa ubongo wake kumpokea mtoto wa jinsia yoyote, kwani pamoja na mipango ya kitaalamu bado yawezekana hitilafu za ushauri/kutozingatia ushauri zikapelekea mtoto wa jinsi isiyotarajiwa kupatikana. Hata hivyo mafundisho ya didi yanatupa faraja kubwa kwamba mtoto anatoka kwa Mungu. Kwamba wapo watu ambao hawakuweza kujaliwa hata mtoto mmoja, hivyo wazazi wanashauriwa kuwapenda, kuwalinda na kuwatimizia watoto mahitaji yao bila kujali jinsia zao.


Makala haya yameandaliwa na wataalamu wa makuzi toka asasi ya C-Sema inayotafiti na kujifunza namna bora za kukuza watoto Tanzania kupitia mifano na tabia bora za malezi toka kote Afrika na Duniani kwa ujumla. C-Sema inataka kuona Tanzania ambayo jamii nzima iko makini katika makuzi, malezi na maendeleo ya watoto wake. Inawezekana!


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Instagram: @sematanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org


1 view

Recent Posts

See All

Комментарии


bottom of page