top of page
  • Writer's pictureNadhira Jiddawi

Jinsi ya kumsaidia mwanao aache kukojoa kitandani

Hata kama mwanao amefundwa na kuelewa kwamba anapobanwa na haja akahitaji kujisaidia lazima aende chooni, usishangae awapo usingizini hasa usiku bado akakojoa kitandani. Kukojoa kitandani ni jambo la kawaida hasa kwa watoto wenye umri chini ya miaka saba. Ifahamike kuwa kukojoa kitandani si jambo la hiari na hivyo halimpi mwanao fursa ya kulidhibiti. Kama ilivyo kuota jino la kwanza la mtoto, kukojoa kitandani hasa usiku ni hatua mojawapo ya kawaida kabisa katika kukua kwa mtoto kimaumbile.


Ingawa kukojoa kitandani huathiri watoto wa jinsi zote, wavulana huathiriwa zaidi ya wasichana na habari njema ni kwamba vitendo hivi huondoka pasi mzazi/mlezi kufanya lolote inapotimu muda muafaka. Madaktari wanashauri kuwa ingawa hapana umri unaokubalika kama sahihi kwa watoto kuacha vitendo hivi mtoto akiendeleza tabia hii baada ya umri wa miaka mitano hadi saba na zaidi mpeleke hospitali kwa uchunguzi wa kitabibu. Vilevile zipo njia kadhaa za kukusaidia kupambana na tatizo hili tunazijadili hapa chini.


Usimwadhibu. Badala ya kugomba na kutumia ghadhabu mweleweshe mtoto kuwa kukojoa kitandani ni jambo la kawaida katika ukuaji na kwamba si yeye pekee kwani watoto wengi tu wa umri wake hupitia kipindi kama hicho. Upo ushahidi wa kitaalamu unaoonyesha kwamba mara nyingine kukojoa kitandani hurithishwa katika familia na koo. Hivyo ukiwa mkweli unaweza kujua kuwa wajomba, akina-mama wadogo/wakubwa na shangazi zako walipitia changamoto hii walipokuwa wadogo. Kwa nini utoe adhabu kwa mtoto kwa jambo asilo na hiari nalo katika kulitenda?


Dhibiti unywaji wa maji na vinywaji. Hakikisha mtoto anapata maji na vinyaji mapema kabla ya giza kujongea ili asiwe na kiu na kutaka kunywa maji karibu kabisa na muda wa kulala. Iwapo anakwenda shule na kurudi jioni mwekee maji katika chupa apate kunywa kidogo-kidogo kutwa nzima. Lengo hapa ni kuzuia kiu kubwa masaa ya usiku na kupunguza ulazima wa kubanwa mkojo awapo usingizini.


Pangilia muda wa kwenda kujisaidia. Hakikisha mtoto anakwenda kukojoa ikiwezekana kila baada ya masaa mawili hata matatu na mara zote kabla ya kwenda kulala. Mtoto akiwa hana chochote katika kibofu chake cha mkojo uwezekano wa kukojoa kitandani unapungua sana.

Usimwamshe usiku kujisaidia. Watalaamu wa malezi wanakubaliana kwamba kumwamsha mtoto akiwa usingizini akakojoe hakumsaidii kujenga mfumo wa kudumu kupambana na changamoto ya kukojoa kitandani. Ingawa lengo ni jema linamnyima mtoto fursa ya kujenga mfumo binafsi wa mwili kuacha kukojoa kitandani. Vilevile ni usumbufu wa aina fulani kwa usingizi mnono anauhitaji mtoto.


Kuvimbiwa yaweza kuwa sababu? Angalia iwapo kuvimbiwa ni sababu ya mtoto kukojoa kitandani. Kawaida (kuvimbiwa) tumbo linapojaa husababisha uwepo wa mzigo juu ya kibofu cha mkojo na kusababisha hitaji la kukojoa mara kwa mara. Hii ikitokea usiku basi uwezekano wa mtoto kukojoa akiwa usingizini huongezeka. Dalili mojawapo ya kuvimbiwa ni kukosa haja kubwa kama ilivyo kawaida yake. Unaweza kupambana na kuvimbiwa kwa kumpa mtoto maji mengi na vinywaji kama juisi ya matunda, nk.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org


1 view

Recent Posts

See All

Comentarios


bottom of page