top of page
  • C-Sema Team

Jinsi ya kuandaa chakula cha nyongeza cha mtoto wa miezi 6

Updated: Aug 30, 2023

Tumezungumza na Bi Neema Shosho, mtaalamu wa lishe toka Shirika la Chakula Duniani (WFP). Bi. Shosho ametupa darasa la namna chakula cha mtoto wa kuanzia miezi 6 kinavoweza kuandaliwa kwani katika umri huu anaweza kula chakula mchanganyiko kutoka katika makundi mbalimbali ya chakula kama; nafaka, mizizi, viazi na ndizi mbichi, wanyama na mazao yake, jamii ya mikunde na wadudu, mbogamboga na matunda na mafuta. Bi. Shosho anashauri usimpe mtoto wa chini ya mwaka mmoja asali, sukari kwa wingi wala chumvi. Ni vyema mzazi/mlezi ukasubiri mtoto afikishe mwaka mmoja ndipo uanze kumpa vitu hivi.


Bi. Shosho anasema umpatie vyakula vya nafaka, jamii ya mizizi na ndizi mbichi kama ugali, wali, mihogo ndizi mbichi, viazi, boga. Vyakula hivi vina virutubisho vya wanga kwa wingi hivyo huupatia mwili nishati lishe. Mzazi / mlezi. KUMBUKA-Nafaka zisizokobolewa kama mahindi (dona), ulezi, uwele, ngano, mchele n.k. zina virutubishi zaidi kuliko zilizokobolewa.

Wanyama na mazao yake (mfano mayai, samaki, kuku, wadudu), karanga, mbegu za alizeti, vyakula jamii ya kunde, maziwa na bidhaa zake vyakula hivi vina protini (utomwili) kwa wingi hivyo husaidia kujenga mwili wa mwanao. Mtoto mdogo anahitaji kundi hili kwa wingi kila siku. Mzazi / Mlezi fahamu kuwa maziwa ya wanyama kama ng'ombe yanampatia mtoto madini ya kalsium kwa wingi ambayo ni muhimu sana kwa ajili ya kujenga mifupa na misuli imara ya mtoto.


Matunda na mboga mboga vinasaidia kuupa mwili wa mtoto vitamini na madini kwa wingi na kumpatia kinga imara ya mwili, vile vile huupa mwili nyuzinyuzi ambazo husaidi mfumo mzima wa tumbo wa usagaji wa chakula. KUMBUKA- Mafuta mazuri ya kula ni yale yatokanayo na mimea kama karanga na mbegu kama mbegu za ufuta, alizeti na maboga. Mafuta haya huupatia mwili wa mtoto nishatilishe kwa wingi na ni mazuri kwa afya.

Mtoto wa miezi 6-8 ambaye ananyonya maziwa ya mama apewe chakula angalau mara mbili kwa siku. Mtoto wa miezi 9-23 anayenyonya maziwa ya mama apewe chakula angalau mara tatu kwa kwa siku. Ni MUHIMU sana kuelewa kuwa mtoto ambaye hanyonyi maziwa ya mama apewe chakula bora na milo kamili angalau mara nne kwa siku ili aweze kukua vizuri.


Bi. Shosho anatoa wito kwako mzazi / mlezi ukumbuke kumpatia mtoto maji safi na salama ya kunywa pamoja na vinywaji kama juisi za matunda za kutengeneza nyumbani kwa maji safi na salama. Hakikisha juisi yako ni nzito nzito na sio maji matupu. Kwa mzazi/mlezi aliyeanza kumpa mtoto maziwa ya ngâombe kabla mtoto hajatimiza mwaka mmoja, Mzazi/mlezi wahi kupata maelekezo kwa wataalamu wa afya namna ya kuyaandaa na kuyatumia maziwa hayo.


Unapoandaa chakula cha mtoto, epuka matumizi ya vitu kama mafuta mengi, chumvi au sukari nyingi kwa kuwa Unahatarisha afya ya mtoto wako. Kwa watoto wadogo wasioweza kutafuna vizuri, mpe vyakula vilivyopondwapondwa kama nyama, samaki, maharage na hata mbogamboga na matunda.


Usimpe mtoto mchuzi mtupu mfano wa maharage, nyama, au mchicha kwa kuwa mchuzi hauna virutubishi vya kutosha. Pondaponda vyakula hivyo na mpatie mtoto wako. Ongeza kiini cha yai kwenye uji au viazi vilivyo pondwapondwa ili kuongeza kiwango cha protini. Wakati uji ukiwa unachemka, vunja yai, weka kiini koroga haraka na hakikisha unaiva vizuri ndipo umpe mtoto. Hakikisha kuwa vyakula ambavyo mtoto hawezi kuvitafuna, unavipondaponda vizuri. Saga kwa kutumia blenda au kinu kisafi kisha andaa.Ongeza vitu kama maziwa au siagi ya karanga katika vyakula vya mtoto. Hakikisha kuwa karanga zimechaguliwa na kuandaliwa vizuri. Kumbuka kuwapatia watoto maji ya kunywa yaliyo safi na salama. Hakikisha humpi mtoto vinywaji vyenye sukari nyingi kama soda, chai na kahawa. KUMBUKA-Mbogamboga na matunda ni muhimu sana. Zitamkinga mtoto dhidi ya magonjwa mbalimbali kama upungufu wa damu, kuugua mara kwa mara na husaidia kupata choo laini na kwa wakati.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org.


0 views

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page