Kuna wakati mama ananweza kushindwa kunyonyesha mtoto kwa sababu zisizoweza kuzuilika, mathalani kifo cha mama, mama mwenye mtoto ambaye si wake au mama mwenye maradhi. Usimnyonyeshe mtoto katika mazingira haya:
Mama ana ugonjwa wa kifua kikuu na hajaanza dawa.
Mama anatumia tiba ya dawa za saratani (chemotherapy).
Mama ana maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Hata hivyo unaweza ukashauriana na daktari kujua njia salalma zaidi ya kufanya kama itabidi uendelee na unyonyeshaji.
Kama unatumia dawa haramu za kulevya kama bangi, heroini, kokeni (cocaine) na n.k. usinyonyeshe.
Kama mwanao ana maradhi yasiyo ya kawaida ya galactosemia na hawezi kuvumilia sukari ya kwenye maziwa (galactose) iliyoko kwenye maziwa. Fuata ushauri wa daktari.
Unapokuwa ukitumia dawa za magonjwa kama parkinson’s, kipanda uso au homa ya viungo (arithritis).
Hata hivyo kuna maradhi ambayo unaweza kuwa nayo na kuendelea na unyonyeshaji kama kawaida kama vile mafua. Baadhi ya magonjwa unayoyapata ukiwa unanyonyesha yatamjengea mwanao kingamwili (antibodies) kupitia unyonyeshaji. Kingamwili hizi zitamsaidia kupamabana na maradhi. Hata hivyo, ongea na daktari kabla ya kuanza / kuendelea kunyonyesha endapo una mpango wa kutumia dawa ya aina yeyote ile akupe ushauri stahiki.
Chama cha madktari wa watoto cha marekani (American Academy of Paediatric) hupendekeza unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee mpaka kufikia miezi 6 na kwamba watoto wanaolazimika kutumia maziwa mengine tofauti na maziwa mama wapewe nyongeza ya madini ya chuma. Dozi hii ya madini ya chuma inatakiwa indelee mpaka mpaka pale atakapoanza kula vyakula vilivyoongezwa madini ya chuma.
Kwa ujumla ni muhimu kuchunguza kiwango cha madini ya chuma kwa watoto wote wenye mwaka mmoja. Katika nyongeza hiyo unaweza pia ukajadiliana na daktari kama kuna uwezekano wa nyongeza ya vitamini nyingine kama vile vitamini D katika ulaji wa mtoto.
Je, zipo sababu za kwa nini baadhi ya mama kushindwa kunyonyesha?
Baadhi ya akina mama huwa wanahofu ya kunyonyesha kwa sababu nyingi na ikiwemo kuhofia mabadiliko katika maumbo ya matiti yao. Hata hivyo ukweli ni kwamba kuna sababu nyingi zinazochangia matiti yao kubadilika kama vile umri, jenetiki, mtindo wa maisha kama vile uvutaji wa sigara na hata nguvu ya uvutano ya dunia (gravity).
Pamoja na hayo akina mama wengine pia hujitetea wakisema kuwa wametingwa na majukumu hivyo wanakosa muda muda wa kutosha kunyonyesha watoto wao wenyewe. Lakini ukweli ni kwamba hakuna lishe inayoweza kulingana na maziwa ya mama na ikumbukwe kuwa maziwa hayo yapo kwa ajili ya wewe kumnyonyesha mwanao na kama sivyo yasingekuwepo.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, Instagram @sematanzania na www.sematanzania.org
Picha ni kwa hisani ya Shutterstock.
Comments