top of page
  • C-Sema Team

Hatupaswi kupata usingizi kwa watoto 10 waliochinjwa Njombe hapahapa Tanzania.Matukio ya watoto wa umri kati ya miaka miwili hadi sita kuchinjwa na kukatwa koromeo, sehemu za siri na ulimi wilayani Njombe hapa-hapa Tanzania si ya kukalia kimya.

Hivi binadamu anatoa wapi ujasiri wa kumteka na baadae kumchinja mtoto wa miaka kati ya miwili hadi sita? Yaani unamkata koromeo, sehemu zake za siri, unanyofoa masikio alafu kama haitoshi unamtoa ulimi? Hii ni hapa Tanzania Mji wa Njombe na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe! Loh!


Mkuu wa Wilaya Njombe Bi. Ruth Msafiri kwa taharuki na hali ya sintofahamu ametoa amri kwa wazazi na walezi kuwapeleka na kuwafuata shule watoto wao. Pia, ameagiza watoto wote wilayani humo kuhakikisha kuwa wanatembelea kwa makundi ili kuimarisha ulinzi baina yao.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka amehusisha mauaji haya na imani za kishirikina pamoja na malipizo ya visasi.


Hebu tuachane na sababu za kwa nini waliuawa. Pata picha kwamba, 'Watoto sita waliookotwa (wakiwa wamekufa) Halmashauri ya mji wa Njombe, wawili walipotea na kuokotwa wakiwa wameuawa misituni, wawili wameokotwa maeneo tofauti wakiwa wamekufa na hawakutambulika na havyo wao walizikwa na halmashauri. Hadithi za wengine zinafanana na hizi. Kisha mtoto wa 10 yeye aliokotwa mtoni Hagafilo huko Njombe.' Hii ni kwa mujibu wa taarifa za mwandishi wa gazeti la Mwananchi.


Katika kipindi hiki cha majonzi hatuna budi pia kutoa pongezi kwa mwalimu wa shule ya msingi mjini Njombe ambaye amenukuliwa akisema, 'Ninafundisha darasa la kwanza, kulingana na umri wao inaniwia vigumu kuwaruhusu kuondoka, kila mtoto anachukuliwa na mzazi wake. Siwezi kukubali hali hii imkute mwanafunzi wangu. Wapo wanakaa mpaka muda mbaya ila mpaka mzazi aje nami ndipo nirudi nyumbani.'


Mwalimu huyu anatufundisha kwamba tunaweza kufanya jambo ndani ya uwezo wetu kwa nafasi tulizokirimiwa na Mungu katika kukemea na kulaani mauaji ya namna hii kamwe yasijitokeze. Inaanza na mimi. Inaanza na wewe.PICHA: Kichwa cha habari hii hapo juu kimetoka kwa mchoraji vibonzo maarufu hapa kwetu Ndugu Masoud Kipanya, yeye alichagiza, 'Hatukupaswa kupata usingizi kwa hili.' Ione Tweet yake HAPA. Sisi tunasema bado tunayo nafasi si tu ya kukosa usingizi, bali pia ya kufanya kila liwezekanalo katika uwezo wetu kupinga tukio hii.

1 view

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page