top of page
  • C-Sema Team

Haki za uzazi katika sheria ya kazi Tanzania hizi hapa


Haki za uzazi ni haki zinazomwezesha mwanamke mwajiriwa kutimiza majukumu yake ya uzazi na kufanya kazi au kuzalisha bila kubaguliwa, kubugudhiwa au kupoteza ajira. Likizo ya uzazi ikiwa ni moja ya haki za uzazi, humpa mama na baba muda kutoa matunzo muhimu kwa mtoto katika siku/miezi ya mwanzo ya maisha yake, ikiwa ni pamoja na kumnyonyesha. Vilevile likizo ya uzazi humpa mama mwajiriwa muda wa kupumzika na hivyo kusaidia mwili wake kurudi katika afya na hali ya kawaida baada ya kujifungua. Kwa mantiki hiyo, ni muhimu mwajiri na mwajiriwa kufahamu vizuri haki hizi na wajibu katika utekelezaji wa sheria.


Toa taarifa. Mwanamke mwajiriwa anapaswa kumfahamisha mwajiri wake nia ya kuchukua likizo ya uzazi angalau miezi mitatu kabla ya tarehe ya makisio ya kujifungua huku akiambatanisha kielelezo cha daktari juu ya ujauzito. Likizo ya uzazi inaweza kuchukuliwa wiki nne kabla ya kujifungua au mapema zaidi iwapo kuna uthibitisho wa daktari kwamba ni muhimu kufanya hivyo kwa ajili ya afya ya mama au mtoto. Mama ana haki ya kupewa likizo ya uzazi sio chini ya siku 84 yenye malipo. Vilevile kwa aliyejifungua mtoto zaidi ya mmoja (mapacha au zaidi) anapaswa kupewa likizo ya uzazi ya siku 100 yenye malipo.


Iwapo mtoto amefariki. Mwanamke ana haki ya kupewa tena likizo ya uzazi ya siku 84 yenye malipo endapo mtoto wake atafariki katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kuzaliwa. Hata hivyo, kisheria, mwajiri anawajibika kumpa mwanamke mwajiriwa likizo nne tu za uzazi katika kipindi chote cha ajira.


Lini arudi kazini. Mama mwajiriwa haruhusiwi kurudi kazini katika kipindi cha wiki sita za mwanzo tangu kujifungua isipokuwa pale tu atakapokuwa ameruhusiwa kufanya hivyo na daktari. Pia anaporudi kazini mama anayenyonyesha ana haki ya kupewa muda wa saa mbili kwa siku wakati wa kazi kwenda kumlisha/ kumnyonyesha mtoto wake.


Kufanya kazi usiku. Mwanamke mjamzito na mama anayenyonyesha hapaswi kupangiwa kazi za usiku kuanzia miezi miwili kabla na baada ya kujifungua, au wakati wowote atakapoonyesha kwa mwajiri cheti cha daktari kinachoeleza kwamba hali yake haimruhusu kufanya kazi usiku.


Likizo ya uzazi kwa baba mwajiriwa. Sheria ya ajira inampa likizo ya siku zisizopungua tatu zenye malipo baba wa mtoto aliyezaliwa. Kwamba siku hizo zichukuliwe katika muda wa wiki moja ya kwanza tangu kuzaliwa kwa mtoto. Kwa kawaida likizo hiyo ya siku 3 hutolewa mara moja tu katika mzunguko wa likizo ya mwaka bila ya kujali idadi ya watoto watakaozaliwa katika kipindi hicho. Yaani likizo hii hutoka mara moja tu kila mwaka hata kama baba ana watoto alowapata zaidi ya mara moja katika mwaka husika.


Likizo inampa baba fursa ya kumhudumia mama na mtoto, kumsaidia mama kujenga msingi mzuri wa kumlisha mtoto na pia kutafuta mahitaji ya familia. Baba wa mtoto aliyezaliwa anaweza pia kupewa likizo isiyopungua siku 4 yenye malipo, wakati wa kuuguliwa na mtoto, kifo cha mtoto au kifo cha mwenzi wake. Likizo hiyo ya siku 4 hutolewa mara moja katika kipindi cha mzunguko wa likizo ya mwaka bila kujali idadi ya matukio yaliyojitokeza katika kipindi hicho. Hata hivyo, mwajiri anaweza kuidhinisha mwajiriwa kuchukua siku zaidi zisizo na malipo kulingana na tatizo alilopata.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

5 views

Recent Posts

See All

Kommentare


bottom of page