Faida za unyonyeshaji kwa mwanao.
Maziwa ya mama humpatia mtoto virutubisho vyote anavyohitaji katika miezi 6 ya mwanzo toka kuzaliwa. Hivyo kufanya maziwa ya mama kuwa lishe muafaka kwa mtoto. Yana uwiano mzuri wa wanga, protini, mafuta, vitamini pamoja na madini. Vilevile maziwa haya yanameng'enyeka vyema kuliko maziwa ya kopo. Maziwa ya mama hupunguza hatari ya mwanao kupata asthma au mzio. Pia yana kingamwili (antibodies) wanaopambana na virusi pamoja na bakteria wanaosababisha magonjwa.
Tafiti zimeonesha kwamba watoto wanaotunzwa kwa maziwa ya mama bila ya lishe nyingine mpaka miezi sita wanaepuka hatari za kupata maambukizi ya ugonjwa wa masikio na magonjwa ya njia ya upumuaji. Maziwa pia yameonekana kusaidia kupunguza hatari ya kupata magonjwa kama kisukari na uzito kupindukia.
Ifahamike kuwa kwamba maziwa ya mama huchangia kuongeza werevu kwa watoto (IQ). Tena maziwa ya mama na kitendo cha kunyonyesha huchangia kutengeneza muunganiko katika mahusiano ya mtoto na mama ambayo hutokana na kule kugusana kati ya mama pamoja na kutazamana wakati wa kunyonyesha na hali hii pia huwafanya watoto kujihisi salama wanapokuwa na mama zao.
Mwisho na muhimu, je wajua kwamba maziwa ya mama husaidia kumpunguzia mwanao hatari ya kupata kifo cha ghafla (sudden infant death syndrome)?
Je, kuna faida zozote za unyonyeshaji kwa mama?
Unyonyeshaji husaidia kutoa kichocheo cha oxytocin ambacho husababisha mji wa uzazi wa mama (uterus) kurudi katika umbo na hali yake ya kawaida kabla ya kupata ujauzito na huweza pia kusaidia kupunguza kutoka damu ukeni baada ya kujifungua.
Unyonyeshaji pia huchangia kuchoma kalories ili kumsaidia mama kupunguza uzito alioupata wakati wa ujauzito ili arudi katika umbo lake la awali mapema iwezekanavyo.
Unyonyeshaji husaidia kushusha hatari ya kupata saratani ya matiti na hata saratani ya mfuko wa mayai (ovarian cancer). Vilevile unyonyeshaji husaidia katika kupunguza hatari ya kupata osteoporoisis.
Mwisho kabisa unyonyeshaji husaidia kupunguza matumizi ya pesa kwani huna haja ya kununua maziwa ya kopo, nk. kwani mama maziwa yake tayari yapo kwa usafi unaotakiwa.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, Instagram @sematanzania na www.sematanzania.org
Picha ni kwa hisani ya Ipp.com