top of page

Dondoo tano kwako mzazi wakati huu wa siku kuu

C-Sema Team

Naam, hizi hapa dondoo tano tulizokukusanyia toka kote mtandaoni ili kukusaidia kuwa na wakati mzuri na watoto wako msimu huu wa likizo. Twatumaini kuwa dondoo hizi zitaifanya likizo yako kuwa ya amani na furaha zaidi.


Malezi wakati wa siku kuu

Huwezi kumfurahisha kila mtu. WebMD, ambao ni madaktari mtandaoni wao wanasema, 'Mtu fulani - mzazi, wifi au mkwe - atakuletea maudhi msimu huu. Lakini mara nyingi watoto hawatakuletea maundhi kwani wao mambo madogo-madogo ambayo watayakumbuka ni pamoja na muda uliotumia kukaa nao kuzungumza, kucheza nao na wakati mwingine ukakaa kimya pembeni ukiangalia wanavyobuni hadithi wakicheza na midoli na kadhalika. Jiweke karibu na watoto wako sasa kwani hivi karibuni watakuwa watu wazima na watahama kwenda kuanza maisha yao wenyewe.'


Kumbuka msongo ulionao unaweza kuleta dhahma kwa watoto wako. Mwanahabari Amy Joyce, Mwandishi wa makala za malezi wa Washington Post anasema, likizo ni wakati unaosababishia wazazi wengi msongo wa mawazo. Kwamba ingawa tunawapenda watoto wetu na wao huleta kwetu furaha nyingi, mara zingine uwepo wao wakati wa likizo hutuongezea msongo wa mawazo. Hata hivyo, tunapaswa kuwa sehemu ya suluhisho kwa kuwapa mazingira ya amani wawapo likizoni pamoja na misongo yetu wazazi. Kamwe tusiruhusu magumu yetu yalete athari kwa watoto wetu.


Tenga muda maalumu katika siku kwa ajili ya watoto wako. "Wazazi wanajikuta wakihangaika huku na kule wakati wa likizo. Wakati mwingine tunasahau kuwa watoto wanahitaji ukaribu wetu zaidi kuliko wakati wowote wawapo mapumzikoni. Tunaweza kutoa zawadi ya ukaribu kila siku, bila kulipia hata senti moja. Utapata amani kama mzazi kujua kuwa muda wako wala si zawadi na pesa ndio unaomletea mtoto furaha zaidi. Dakika chache hizo huweza kujenga msingi wa mahusiano kati yetu na watoto, na kuonyesha upendo zaidi kuliko mizawadi tunayohangaika nayo." Dk Kevin Arnold katika Psychology Today anasema.


Dhibiti matarajio ya zawadi. "Tumekubaliana zawadi tatu kila mtu kwa ajili ya Krismasi, na hakuna zaidi. Watoto wetu wanajua kutarajia hili, ambapo inamaanisha wanajua kuna kiwango cha mwisho cha zawadi wanazoweza kutarajia. Familia nyingine nyingi hujiwekea nadhiri ya zawadi zinakuja kwa namna hii: 'anachotaka mtoto, hitaji lake halisi, nguo na vitabu'. Vyovyote vile utakavyo ni hulka njema kujiwekea mipango ya zawadi, kuwasiliana na kukubaliana na watoto wetu kujiwekea ukomo. Hii husaidia kuweka matarajio ya kweli."


Jipe raha mwenyewe. Kituo cha Rasilimali cha Mzazi cha SCAN kinatuambia yote, "Kumbukumbu mbaya za msimu uliopita wakati mwingine zinazuka wakati wa likizo, mara nyingi zinaongeza matatizo zaidi. Hakikisha unakuwa na watoto wako kwa amani na salama - kaa na ndungu, jamaa na marafiki mnaorandana kimitazamo. Ndugu wa 'kweli' mnaosaidiana katika raha na hata dhiki. Kuwa na watu wengine kunaweza kutoa mwanya wa kuleta mazingira yaso-rafiki. Huu ni wakati wako na wanao kuandika historia - hivyo toka, kakutane na watu, jichanganyeni na kujenga historia au kumbukumbu nzuri katika nyoyo za familia yako.


Kwa kuwa hii inaweza kuwa makala yetu ya Mwaka Mpya tunataka kuwakumbusha kwamba jambo bora zaidi kwa cmtoto wako likizo hii ni kutumia muda wako pamoja naye. Kama Muamerika mwenye asili ya Afrika, Frederic Douglass alivyopata kusema 'Ni rahisi kujenga watoto wenye nguvu kuliko kutengeneza watu waliporomokewa maadili.'


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

0 views
bottom of page