top of page
  • C-Sema Team

Athari za Matumizi ya Vifaa vya Kielektroniki kwa Watoto

Updated: Aug 30, 2023


Kila mmoja wetu ni shahidi kwamba mabadiliko ya teknolojia yameleta athari hasi na chanya katika nyanja tofauti za maisha ya kila siku ya mwanadamu. Katika mabadiliko haya rika zote zimeguswa ikiwemo watoto. Watoto hufurahia matumizi ya vifaa vya kielektroniki kutokana na michezo (gemu) mbalimbali inayopatikana katika vifaa hivyo ikiwemo simu za mkononi, runinga na tablet. Pamoja na kwamba watoto hufurahia gemu kuna athari kubwa katika ukuaji wa ubongo itokanayo na kutumia muda mwingi kutizama kioo (screen) katika umri mdogo sana na kwa muda mrefu.


Ubongo wa mtoto hukua na hujengeka haraka zaidi akiwa na umri mdogo kuanzia kuzaliwa hadi umri wa miaka mitatu. Tafiti zimebainisha kuwa hiki ni kipindi muhimu sana kwa mtoto kupata muda wa kutosha kuwa karibu na watu wanaomzunguka. Mahusiano ya karibu na watu na mazingira ndiyo husaidia sehemu ya ubongo wa mbele (frontal lobe) kukua kikamilifu katika kipindi hiki. Kwa bahati mbaya imekua ni kawaida, hasa mijini, kuona watoto wadogo kabisa simu ziwaliwaze badala ya kuliwazwa, kucheza na wazazi wao na kupatiwa mawasiliano ya ana kwa ana ambayo yanasaidia ukuaji wa sehemu ya mbele ya ubongo amabayo ni rasmi kwa kazi ya utambuzi (cognitive functioning).


Wataalamu wa masuala ya saikolojia na ukuaji wa watoto wanabainisha kuwa, simu janja na tablet zimechukua nafasi kubwa ya michezo ya nje na kuwafanya watoto kushindwa kujifunza kwa kutopata muda wa kuchangamana na wenzao ili kujifunza umoja, huruma, hisia na stadi za maisha. Hii hupelekea watoto kuwa tegemezi wakiwa na umri wa kujitegemea mambo madogomadogo kutokana na athari katika mfumo wa ubongo uliosababishwa na matumizi ya vifaa hivi.


Tafiti zinaendelea kuonesha kuwa, gemu za kwenye vifaa vya kielektroniki zinaathiri ubunifu, udadisi na uwezo wa kufikiri kwa watoto. Katika ukuaji wa ubongo, kuna mchakato wa upukutishaji wa seli mfu unaofanywa na muundo upelekao mawasiliano baina ya neva. Pale mtoto anapotumia muda mwingi kuangalia gemu na kutoshughulisha ubongo na mambo mengine, muundo huu hupukutisha seli zinazohitajika kuchochea ubunifu na udadisi wa mtoto baada ya kutotumika muda mrefu kwa kazi yake lengwa. Hii huathiri moja kwa moja mfumo wa ukuaji wa ubongo na uwezo wa kubuni na kudadisi.


Mtoto anapotumia muda mwingi kutizama kioo na kuchezea gemu ambazo tiyari zimeshatengenezwa, akili yake inalala na kudumaa kila kitu kinakuwa kipo tayari kimefanywa kwa ajili yake, hivyo hapati fursa ya kutumia akili yake kuchanganua na kuchunguza mambo. Pia hawezi kuuliza maswali na kudadidisi mambo kwani kila anachokihitaji anabonyeza au anagusa kioo.


Utumiaji wa vifaa hivi hudhoofisha uwezo wa kujifunza kutambua vitu na viumbe vinavyomzunguka, huchelewa kuzalisha misamiati na kujifunza lugha kwakuwa hafanyi mawasiliiano na watu, hupelekea unyonge na msongo wa mawazo kwasababu muda mwingi hapati kuchangamana na watu.


Vilevile, utumiaji wa vifaa vya kielectroniki husababisha tatizo la uoni hafifu kwakuwa huharibu nuru ya macho pale mtoto anapocheza na vifaa hivyo katika umri mdogo na kwa muda mrefu.


Ubongo wa mtoto unapaswa kuwaza jambo moja baada ya jingine taratibu sana ili kumpa muda wa kupambanua na kujifunza hatua kwa hatua; lakini simu janja na tableti zina mambo mengi kwa wakati mmoja ambayo huulazimu ubongo wa mtoto kufanya kazi mara mbili ya uwezo wake. Hii ni hatarishi kwa afya ya ukuaji wa ubongo wa mtoto na hasa huathiri tabia za mtoto.


Athari hizi hazimaanishi tusiwe na vifaa hivi majumbani kwetu au watoto wasifurahie teknolojia. La hasha! Bali tuwasimamie vyema wanapotumia vifaa hivi na kuwapangia muda maalum pamoja na kuwaongoza kuangalia michezo yenye kujenga ubunifu, kuchochea tabia njema na kuelimisha. Pia inashauriwa kutenga muda wa familia kwa kutizama pamoja nao michezo inayowafurahisha, kuwa na muda wa kula pamoja na kuzungumza nao mara nyingi.


Kisayansi inashauriwa kuwa mtoto wa umri wa chini ya miaka miwili asiangalie ama kutumia vifaa vya kielectroniki kabisa, miaka miwili na kuendelea inashauriwa kutumia na kuangalia vifaa hivyo kwa muda usiozidi masaa mawili kwa siku kwa kupumzika na kucheza michezo mingine na kuchangamana na watu kila baada ya nusu saa.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

17 views

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page