Kuna swali ambalo watu wengi hupenda kuuliza kupitia Huduma ya Simu kwa Mtoto, namba 116. Utamjuaje mtu anayeweza kumkatili mtoto kingono? Kwa ufupi, hakuna alama ya mkatili. Mtu yeyote ana uwezo wa kumkatili mtoto hivyo haiwezakani kumtambua mtu anayemkatili mtoto kingono kwa kumuangalia tu. Vilevile, ukatili wa kingono unahitaji umakini sana kuutambua.Tafiti zinaonyesha kuwa mara nyingi watu wanowakatili watoto ni watu wao wa karibu kama vile ndugu hasa wale wanaoishi nao nyumba moja, waalimu, majirani, n.k.
Almuradi mzazi amemuamini mtu huyu kiasi kwamba hawezi kuhisi jambo lolote la hatari awapo na mtoto. Mtu huyu ana nafasi ya kumkatili mtoto iwapo atanuia. Wakati mwingine mzazi mwenyewe ndiye anayemkatili mwanae, kitu ambacho hudhihirisha kuwa mtu yeyote huweza kumfanyia mtoto ukatili wa kingono.Mambo mbalimbali huchangia watu kuwakatili watoto. Wengine walilelewa katika mazingira ya kukatiliwa wakiwa wadogo.
Vilevile, kumpa mtu uhuru wa kujenga urafiki wa karibu sana na mwanao huweza kuwa mwanya wa mtoto kukatiliwa na mtu huyu hasa pale mzazi unaposhindwa kuchukua nafasi yako ya kumlinda na kumuelimisha mtoto kuhusu ukatili dhidi yake na namna anavyoweza kujikinga na watu wabaya wanaowadanganya na hatimaye kuwakatili watoto.Pamoja na kwamba ni vigumu kumfahamu mtu anayekatili watoto, mara nyingi watoto wenyewe huonyesha dalili mbalimbali wakiwa wamefanyiwa ukatili. Iwapo unamfahamu mwanao vizuri, utaweza kuona mabadiliko madogomadogo katika tabia zake ambazo huenda zikawa dalili kuwa amefanyiwa ukatili. Dalili hizi hutofautiana kulingana na umri na tabia za mtoto.
Mtoto aliyefanyiwa ukatili wa kingono anaweza kujitenga na wenzake, kuwa mpweke, na ghafla hubadilika kuwa muoga sana isivyo kawaida yake. Baadhi ya watoto waliofanyiwa ukatili wa kingono hujaribu kadiri ya uwezo wao kuzuia watu kuona sehemu zao za siri, kama bado wanaogeshwa. Yaani mtoto atakataa usimnawishe/kumgusa sehemu za siri, au ataonekana kuumia pale unapojaribu kumnawisha na huenda akakataa kuogeshwa kabisa.Mara nyingi, mtoto aliyefanyiwa ukatili hushtuka ama kufedheheka kila akimuona mtu aliyemfanyia ukatili hata kama alikua amemzoea sana.
Dalili nyingine ni kuogopa giza, kushtuka usingizini, mara nyingine anakuwa na jina jipya la sehemu za siri. Pia kukojoa kitandani kama alikuwa hakojoi na wengine hunyonya kidole. Kwa watoto wakubwa zaidi, huweza kujaribu kujinyonga, kukimbia nyumbani, kupata msongo wa mawazo na mengine mengi.Silaha kubwa dhidi ya ukatili kwa mtoto ni ukaribu na mzazi/mlezi. Kama anaweza kuongea, zungumza nae; mdadisi kwa maswali ili kujua kama ametendewa chochote bila wewe kujua.
Mtoto akiwa huru/karibu na wewe atakueleza kila kitu kinachomtatiza kwa kuwa wewe ni zaidi ya mzazi na ni rafiki yake.Fahamu kuwa watu wanaowakatili watoto ni wajanja sana na wanajua kuwa wanachokifanya sio sahihi na hivyo huwatishia watoto kuwa wakisema watawaua au kuwadhuru wapendwa wao. Wengine pia huwafanya watoto wajisikie kuwa wao ndio wamefanya kosa, hali ambayo huwafanya watoto wawe waoga kutafuta msaada kwa mtu mwingine.
Ukihisi kuna kitu kimebadilika kwa mwanao ni lazima uwe makini na uchunguze kwa hekima bila papara wala kumtishia mtoto. Muulize taratibu kile unachokihisi na kumwonyesha kuwa unampenda. Endapo utakuta kweli mtoto amefanyiwa ukatili, hakikisha anaelewa kuwa yeye hana makosa.Kumbuka kuwa ni vyema kuzingitia uangalizi na ukaribu na watoto wako ili jambo lolote likitokea, uweze kugundua mapema kabla mtoto hajapata madhara makubwa.