top of page
  • C-Sema Team

TAMKO LA C-SEMA (SIMU YA HUDUMA KWA MTOTO) KUPINGA UKATILI WA WATOTO MTANDAONI 31.05.2018



C-Sema ni taasisi inayoendesha Kituo cha Huduma ya Simu kwa Mtoto kwa kupitia namba 116. Namba 116 ipo kwa ajili ya kupokea taarifa mbalimbali zinazohusu maslahi ya mtoto na kutoa ushauri wa namna ya kuzitatua. Pia tunapokea taarifa zinazohusu ukatili kwa watoto. Hivi majuzi kuna taarifa za kufanyiwa ukatili wa kingono watoto wakike wa darasa la saba shule ya St. Florence ambao picha zao zimekuwa zikisambaa mitandaoni wakiwa na Mwalimu anaeshutumiwa kuwafanyia ukatili huu.


Kusambaza picha hizi ni kosa kisheria na kama taasisi ya kuzuia ukatili kwa watoto tunapinga vikali usambazaji wa picha za watoto mitandaoni hasa katika muktadha wa ukatili wa kingono kwa kuwa kufanya hivyo kunawadhalilisha watoto pamoja na familia zao. Mbali na hivyo hakuna ushahidi ulothibitishwa kuwa watoto wote walio kwenye picha zinazosambazwa wamefanyiwa ukatili huu na kusambaza picha zinazoonyesha sura zao iwe wameathirika au la itawaathiri kwa namna moja ama nyingine. Vilevile, bado haijathibitika kwamba ni kweli watoto wamefanyiwa kitendo hicho na kila mtuhumiwa hata wa ukatili kwa watoto anayo haki mpaka pale itakapothibitishwa kuwa ametenda kosa.


Tungependa jamii ijue kwamba kila picha ama video yenye maudhui ya unyanyasaji wa kingono kwa mtoto au unyanyasaji wa aina yoyote inapopakiwa, inaposambazwa au inapotazamwa, mtoto huyo huathirika na unyanyasaji huo upya. Huyu ni mtoto alie hai na amepitia ukatili wa kutosha. Watumiaji wa mitandao nchini Tanzania wanaweza kusaidia kulinda watoto walioathirika na unyanyasaji wa kingono au ukatili mwingine wanapokumbana nazo mtandaoni na kutokuzisambaza zaidi.


Wengi huona fahari kuwa wakwanza kupakia picha au video hizi kwenye Whatsap, Instagram, Facebook na popote pale kwenye mitandao ya kijamii bila kujua kuwa hili ni kosa kisheria. Sheria mbili za Tanzania zinatoa adhabu, Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na Sheria ya Makosa ya Kimtandao mwaka 2015. Sheria ya Mtoto ya 2009 inasema ni marufuku kupakia, au kuchapa picha au video ya mtoto zinazohusu ukatili awe hai au ameaga dunia. Kisaikolojia binadamu wanajifunza vitu kwa kuiga kile kinachogusa mihemko yao na kukishuhudia kwahiyo hatuwafundishi watu kwa kuwaonyesha video au picha zenye maudhui ya kikatili bali tunapozisambaza tunaendeleza ukatili ilihali ulinzi wa mtoto ni jukumu letu sote.


Jamii ifahamu kwamba kila picha au video ya mwathirika inapotazamwa, mtoto huyu hufanyiwa ukatili upya kwahiyo kabla haujatuma picha au video ni vyema kuwaza je ninamlinda huyu mtoto na familia yake? Na je, jamii itajifunza nini kwa kutazama picha hii? Kumbuka, picha zina madhara kuliko mafundisho. Tupo kwa ajili ya kuwalinda watoto na sio kuwakatili upya.


Tunaomba wale wote waliopakia picha za watoto wa St. Florence wakiwa na Mwalimu wao au wakiwa peke yao kuziondoa mara moja mtandaoni na kutoendelea kuzisambaza tena kwa maslahi ya watoto pamoja na famila zao na kwa maslahi ya watoto wote wa kitanzania. Jukumu la ulinzi wa mtoto ni letu sote, tuwajibike.


Kwa Maelezo Zaidi:

Wasiliana na: Bi. Thelma Dhaje, Meneja wa Kituo cha Huduma ya Simu Kwa Mtoto Tanzania Bara: Thelma.criss@sematanzania.org, (+255) 78709055.


KUHUSU HUDUMA YA SIMU KWA MTOTO Huduma ya Simu kwa Mtoto husaidia watoto wanaohitaji huduma na ulinzi kupitia nambari ya simu 116 bila malipo NA kueleza mahitaji ya watoto kwa watunga sera na watoa huduma za watoto nchini Tanzania. Huduma ya 116 ni bure na inapatikana kupitia mitandao yote Tanzania Bara na Zanzibar.


Kwa maoni na ushauri kuhusu masuala ya watoto na malezi tupigie simu namba 116. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org


1 view

Comments


bottom of page