top of page
C-Sema Team

#SimuliziZa116: Ndoa ya kulazimishwa yapatiwa ufumbuzi

Tarehe 6 Agosti 2018 tulipokeaa simu kutoka kwa msamaria mwema aishie wilayani Mpwapwa, alitusimulia kisa cha binti wa miaka 16 aitwaye Dora (sio jina halisi) binti huyu alikatishwa masomo yake ili aolewe.



Binti huyo aliishi na mama yake na kaka yake ambao ndio wamekua wakimsumbua kumlazimisha kuolewa kitendo ambacho ni kuinyume cha haki za watoto. Kitendo hiki kilimsukuma msamaria mwema huyo kuchukua hatua na kutupigia simu bila malipo kupitia nambari 116 kutueleza madhila ya binti huyo.


Baada ya kusikiliza kisa hicho mtoa huduma wetu aliamua kumtafuta Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Mpwapwa ili afanyie uchunguzi suala hilo. Afisa huyo alifika mpaka nyumbani alipokua akiishi binti huyo na kugundua kuwa taarifa ile ilikua ya kweli.


Afisa huyo aliamua kushirikisha serikali za mitaa pamoja na Jeshi la Polisi kwa ajili ya msaada zaidi. Waliwakamata mama na kaka yake Dora na kuwafikisha kituo cha polisi na kuwafungulia mashtaka ya kukiuka haki za watoto kwa kumlazimisha Dora kuolewa na kumkatisha masomo yake.


Kwa wastani, wasichana wawili kati ya wasichana watano wataolewa kabla ya kutimiza miaka 18 hapa Tanzania, (TDHS 2012). Kuwa na uwezo wa kusema uolewe wakati gani na nani akuoe ni haki ya msingi kwa kila binti. Tusikae kimya tukijua mipango hii inaendelea mtaani na vitongojini mwetu. Wasiliana nasi kupitia nambari 116 bila malipo tuzungumze.

1 view
bottom of page