top of page
C-Sema Team

#SimuliziZa116: Mtoto Salma asifirishwa toka Ngara na kutelekezwa barabarani Kilosa

Yalikuwa majira ya jioni kunako saa 1:35 usiku tulipopokea simu kutoka Kilosa mkoani Morogoro, Msamaria mwema atoa taarifa katika Kituo cha Huduma ya simu kwa mtoto kupitia namba 116 na kutanabaisha kuwa alimkuta msichana mwenye umri wa miaka 14 aliyejitambulisha kwa jina la Salma (Jina si halisi) kando ya barabara pindi alipokua njiani akitokea Morogoro mjini kuelekea Kilosa.


Kimsingi, huu ulikua ni usiku wenye kiza kinene hususan kwa binti wa umri mdogo kuwa peke yake katikati ya msitu mkubwa na hivyo Msamaria huyo alishindwa kujua afanye nini juu ya butwaa hilo ingawa alitamani sana kumsaidia binti huyo. Katikati ya tafakuri nzito, alipata maamuzi ya kuijaribu namba 116 ili kuona ni namna gani angeweza kupatiwa msaada wowote.

Kwa bahati nzuri, alipata kuzungumza na mshauri wa Huduma ya simu kwa mtoto ambaye nae bila kuchelewa alimuomba Msamaria huyo ampatie binti simu ili azungumze nae. Mazungumzo kati ya Mshauri wa watoto na binti yalichukua dakika kadhaa ambapo lengo hasa lilikua ni kutaka kupata taarifa na maelezo ya kina kutoka kwa binti mwenyewe.

'Natokea Wilaya ya Ngara, kata ya Kasanga jirani na mpaka wa Tanzania na Burundi. Nilichukuliwa kutoka kijijini kwetu na kuletwa mkoani Morogoro kwa minajili ya kufanya kazi za nyumbani. Pindi nilipowasili Morogoro mjini, mwanaume aliyekuwa na bodaboda alifika na kunichukua kutoka kwenye Kituo cha mabasi na kunipeleka mahali ambapo sikuweza kupatambua, nilijarabu kumuuliza tunaelekea wapi ingawa yeye aliishia kuniamuru nikae kimya na hivyo nikaona nifuate masharti yake. Tulipofika kwenye misitu hii alisimamisha pikipiki na kuniambia niteremke kisha akaniomba nimpatie mawasiliano (namba za simu) ya ndugu zangu, nilimpatia karatasi yenye mawasiliano ya watu wote wa karibu na wa haraka ambao ningeweza kuwapigia. Nilishikwa na bumbuazi kwa kile ambacho sikukitegemea kwani mwanaume huyo aliichuka karatasi yenye mawasiliano hayo, akawasha pikipiki na kuondoka kwa kasi sana. Mwanzoni nilifikiri kuwa mwanaume yule angeweza kurudi ila mpaka sasa ni masaa lukuki yameshayoyoma bila kurejea na hapo ndipo kaka huyu aliponikuta nimesimama peke yangu na kwa uoga mkubwa kwakuwa mahali hapa pamegubikwa na giza totoro na sikujua nini cha kufanya na wapi nielekee.'

Binti huyo alisimulia Kwa kuwa ilikua usiku na msamaria huyo alikuwa na haraka ya kuwahi anakoelekea, Mshauri alimuomba atafute Kituo cha Polisi kilichopo karibu yao kwa minajili ya kuhakikisha kwamba mtoto anakua salama. Baada ya muda mfupi walifanikiwa kuwasili katika Kituo cha Polisi cha Kimamba, kunako majira ya 2:05 usiku mshauri wa Huduma ya Simu kwa Mtoto kupitia namba 116 alipata kuzungumza na Afisa wa Polisi aliyekuwepo katika Kituo hicho muda huo. Baada ya majadiliano ya muda mrefu kati ya Afisa na mshauri, wote kwa pamoja walifikia hitimisho la kumtafuta mtu sahihi wa kumhifadhi binti japo kwa usiku mmoja.

Walimchukua binti na kumpeleka kwa mama mmoja anayejulikana sana kijijini hapo ambae pia ni Mjumbe wa Nyumba 10 ndani ya kijiji hicho. Mama alikubali kumpokea na kumhifadhi mtoto ili mradi kwamba pande zote mbili zitafanya kazi ya kutafuta ufumbuzi na namna ya kumrejesha binti kijijini kwao. Washauri wa Kituo cha Huduma ya Simu kwa Mtoto pia walipata nafasi ya kuzungumza na mama huyo na walimuahidi kufuatilia mwenendo wa suala hilo kwa karibu na pia walijaribu kumueleza namna taratibu zote zitakavyokwenda na kwamba inaweza kuchukua muda kwa mtoto kuunganishwa na ndugu zake na hivyo anapaswa kuwa na subira katika kipindi chote cha uangalizi wa mtoto, mama alikubali na kuahidi kutoa ushirikiano na hivyo mtoto akawekwa chini ya uangalizi wake.

Washauri wa Kituo cha Huduma ya Simu kwa Mtoto walipata kuwasiliana na Afisa Ustawi wa Wilaya ya Morogoro mjini ambaye nae aliwaunganisha washauri hao kwa Afisa Ustawi wa Wilaya ya Kilosa ambae pia alionyesha ushirikiano mkubwa pale alipoamua kwenda kumtembelea binti ili kupata taarifa zaidi. Binti aliarifu kuwa baba yake ni fundi pikipiki kunako mtaa wa Chivu uliopo Ngara mjini na kwamba endapo mtu atamchukua na kumpeleka hadi stendi ya mabasi huko Ngara basi itakua rahisi kwake kupatambua nyumbani kwao ili aunganike na familia yake. Washauri wa Huduma ya Simu kwa Mtoto kupitia namba 116, Polisi sambamba na Maafisa Ustawi wa Morogoro, walifanya kazi kwa pamoja katika kuhakikisha kuwa Salma anafikishwa nyumbani kwao salama salimini. Aidha, Afisa Ustawi wa Ngara alijuzwa taarifa zote zilizomhusu Salma ili nae kwa namna yake aweze kutoa msaada wa kijamii zaidi ukihusisha kuhakikisha kuwa Salma anarudishwa shuleni ili aendelee na masomo.

Mara ngapi umekutana na mtoto / watoto usiku wakiwa hawana uangalizi wa mtu mzima na wewe ukawapita tu ukidhani ni maisha yao? Yawezekana kabisa kuchukua hatua kama alivyofanya huyu msamaria ukaokoa maisha ya mtoto / watoto. Tupigie namba 116 kwa pamoja tuwalinde watoto wetu.

Picha na Yusuf Evli waUnsplash

0 views
bottom of page