Ilikuwa ni siku ya tarehe 2 Januari 2018 ambapo mshauri wetu wa Huduma ya Simu kwa mtoto alipokea simu ya mama kutoka wilaya ya Ubungo. Mama huyu alikuwa na malalamiko ya kukosa matunzo ya mtoto kutoka kwa baba yake. Mama alisema, 'Mzazi mwenzangu hatoi matunzo kwa mtoto wetu tangu alipozaliwa mpaka sasa amefikisha umri wa mwaka mmoja'. Mshauri wetu aliuliza kama kuna hatua yoyote aliyowahi kuchukua kabla ya kupiga #116 na mama akaeleza kuwa hakuwa amechukua hatua yoyote.
Mshauri wetu aliwasiliana na Afisa Ustawi wa Jamii wa wilaya ya Ubungo na kumueleza juu ya tatizo la mama la kutelekezwa pamoja na mwanae. Afisa Ustawi alishauri kuwa mama afike ofisi ya Ustawi wa Jamii wilaya ya Ubungo siku ya tarehe 5 Januari.
Ilipofika tarehe 5 Januari mshauri wetu aliwasiliana na mama aliyekua na furaha kwa kuwa alifanikiwa kupata msaada kutoka kwa Afisa Ustawi wa Jamii. Alieleza kuwa Afisa Ustawi alizungumza na wazazi wote wawili na kumuelewesha baba mtoto juu ya majukumu yake ya malezi kwa mwanae na kuwa kinyume na kutofanya hivyo anaweza kushtakiwa kisheria.
Baba mtoto alikiri kutowajibika kwa malezi kwa kipindi chote cha mwaka mmoja na kuahidi kuwa sasa yupo tayari kuwajibika kama baba na mlezi wa mtoto na yupo tayari kutoa matunzo kwa mtoto wake kila mwezi. Mama alifurahia sana msaada alioupata kupitia Simu ya Huduma kwa mtoto #116.
Huduma ya Simu kwa Mtoto kupitia namba inaendelea kusikiliza na kufikia watoto wengi zaidi hata sasa. Akina mama wengi walotelekezewa watoto wanapata msaada kupitia huduma hii. Tafadhali piga namba #116 sasa uzijue huduma za mtoto hapa Tanzania ama uweze kushiriki kumuokoa mtoto aliye katika mazingira magumu. Mwambie rafiki tufanye jamii kuwa bora zaidi kwa malezi ya watoto wetu. Inawezekana. #Malezi #SimuliziZa116 #116Stories
Comments