Tarehe 13 Juni 2018, msamaria mwema alipiga simu namba 116 - Huduma ya Simu kwa Mtoto akiripoti kisa cha mtoto wa msichana aitwaye Irene* (sio jina lake halisi), mwenye umri wa miaka 10 ambaye anaishi na bibi yake kata ya Ipuli, Manispaa ya Tabora.
Irene anasoma darasa la kwanza kwenye mojawapo ya shule za msingi (jina tumelihifadhi) katika kata ya Ipuli. Huyu msamaria mwema alieleza kuwa wazazi wa Irene wanaishi Bukoba huku bibi akiwa ndiye mlezi mkuu wa mtoto. Kwamba bibi anampiga, kumtukana na imefikia hatua ambapo anamtengea Irene chakula chooni. Mtoto huyu hulazimika kula chakula hicho chooni penye harufu mbaya na nzi wanaovuma wakitaka sehemu ya chakula chake! Vitendo hivi vilimnyima usingizi na uvumilivu msamaria huyu ikabidi atupigie.
Nimewiwa kumsaidia huyu binti ambaye anafanyiwa visa karibia kila siku tena na bibi yake. 'Naombeni usiri wa taarifa hii maana bibi mtu akijua tutakosana, sisi ni majirani.' Alisema msamaria.
Tuliwasiliana na Afisa Ustawi wa Jamii Kata ya Ipuli ambaye mara moja alianzisha uchunguzi uliothibitisha kuwa msamaria alitupa taarifa za kweli. Tarehe 23 mwezi Julai 2018 Afisa Ustawi wa Jamii alitupa mrejesho kwamba mtoto Irene yuko katika mikono salama kwani baada ya mawasiliano na wazazi, ndugu na jamaa zake, amepata makazi mapya ambayo Afisa Ustawi wa Jamii aliridhia kuwa ni salama kwa mtoto Irene.
Huduma ya Simu kwa Mtoto inapatikana kote nchini kwa kupiga simu namba 116 bila malipo tena taarifa zako 'msamaria' zinachukuliwa kwa usiri mkubwa ili kuhifadhi 'mahusiano yako na jirani' unayemripoti. Usikae kimya uonapo mtoto akipitia visa namna hii.
Tupigie simu namba 116 tuzungumze!