top of page
  • C-Sema Team

#SimuliziZa116: DNA yasaidia kumtambua baba mzazi


Ilikuwa tarehe 8 mwezi Januari 2018 tulipokea simu toka kwa Mama Jackson (jina halisi tumelihifadhi) anayeishi Makambini wilaya ya Momba. Mama huyu alitupa taarifa kwamba yeye na mzazi mwenzie walianza mahusiano ya mapenzi mwaka 2015 na walipenda kwelikweli. Bila kutarajia alipata ujauzito mwaka 2016 na kujifungua Januari ya 2017. Mtoto wao alizaliwa na ualbino. Baba alimkataa kwamba si wake sababu eti kwao baba hakuna tatizo hilo.


Baba Jackson ni mwanajeshi na hivyo ilimwia ngumu kumsihi hata kutumia serikali za mitaa ili walau atoe matunzo kichanga Jackson! Baada ya miezi kadhaa ya mapambano hatimaye Baba Jackson alikubali kwa shingo upande kumuanzishia mzazi mwenzie biashara ya duka dogo ili aweze kujipatia kipato kumtunza mtoto.


Biashara ilfana kiasi kwamba Baba Jackson alitaka amrejeshee pesa zote za faida na Baba Jackson hatimaye alifanikiwa kulifunga duka kwa kuuza kila kilichokuwemo kwani bado alisema hakuna haja ya kumsaidia mtoto asiye kuwa wa kwake.


Baada ya kutusimulia madhila haya, siku hiyo hiyo ya tarehe 8 Januari 2018 tulipeleka taarifa hizi kwa Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Songea ambaye alimtafuta Baba Jackson pasi na mafanikio. Afisa Ustawi aliamua kuipeleka kesi hii mahakamani na ilipangiwa kusikilzwa Jumatatu Januari 15, 2018.


Mahakamani Baba Jackson alimkana mtoto na kudai kipimo cha DNA kuthibitisha uhalali wa yeye kuwa mzazi. Hatimaye kipimo cha DNA kilifanyika na kuthibitisha kwamba yeye - Baba Jackson ni baba halali wa mtoto. Mahakama iliamuru atoe matunzo ya kiasi cha shilingi 50,000 kila mwezi kama sehemu ya gharama za matunzo ya mtoto. Baba Jackson anatoa matunzo hadi sasa.


Huduma ya Simu kwa Mtoto kupitia namba inaendelea kusikiliza na kufikia watoto wengi. Akina mama wengi walotelekezewa watoto wanapata msaada kupitia huduma hii. Tafadhali piga namba #116 sasa uzijue huduma za mtoto hapa Tanzania ama uweze kushiriki kumuokoa mtoto anayepitia wakati mgumu. Mwambie rafiki tufanye jamii kuwa bora zaidi kwa malezi ya watoto wetu. Inawezekana. #Malezi #SimuliziZa116 #116Stories

1 view

Recent Posts

See All

Comments


bottom of page