top of page
C-Sema Team

#SimuliziZa116: chakula kipi chafaa mtoto wa mwaka mmoja?

Tarehe 7 Agosti 2018 tulipokea simu kutoka kwa Baba Jumanne (jina lake halisi limehifadhiwa kwa madhumuni ya faragha) mkazi wa Wilaya ya Kahama akiomba msaada wa aina ya chakula kwa ajili ya mtoto wake Jumanne mwenye umri wa mwaka mmoja.


Mtoa huduma wetu alimshauri kuwa ingawa mtoto wake bado anahitaji kuendelea kunyonya maziwa ya mama, maziwa ya mama pekee hayatoshelezi mahitaji ya kilishe kwa mtoto aliye zaidi ya umri wa miezi 6. Endapo mtoto atacheleweshwa sana kuanzishiwa chakula cha nyongeza atashindwa kukua vizuri.


Alimshauri kumpatia vyakula vyenye protini kama maziwa, mayai, jibini, maharage, soya, nyama na samaki. Aina hii ya vyakula husaidia katika ukuaji na huzuia mtoto kudumaa. Mwongozo mpya wa Wizara ya Afya (November 2014) unaeleza kuwa watoto wenye umri wa mtoto Jumanne (chini ya mwaka mmoja) wasipewe karanga kwani karanga zimechangia kwa kiasi kikubwa tatizo la mzio wa chakula (food allergy).


Baba Jumanne alielezwa umuhimu wa uji na vyakula vya wanga mfano mahindi, ulezi viazi, mchele na mtama. Kwamba vyakula hivi huupa mwili nguvu na joto kumuwezesha mtoto kuwa mchangamfu.


Alielezwa juu ya mwongozo mpya wa Wizara ya Afya (November 2014) unaoelekeza watoto wenye umri chini ya miaka 5 wasitumie dona - kwani dona ina makapi lishe mengi yanayozuia uvyonzwaji mzuri wa madini chuma mwilini, pia inafanya watoto wasiongezeke uzito vizuri kwani dona inampatia mtoto nishati lishe hafifu. Makapi lishe yanayotokana na matunda na mbogamboga yanatosha kama mbadala wa makapi lishe ya dona.

Mtoa ushauri alimshauri Baba Jumanne kuhakikisha kuwa mtoto anapata matunda na mboga mboga ambazo husaidia kutoa kinga kwenye mwili pamoja na kuakikisha mtoto anapata kiwango sahihi cha maji kwa siku.


Mwongozo mpya wa Wizara ya Afya (November 2014) unaelekeza namna ya kuwapatia lishe bora watoto wenye umri chini ya miaka 5. Usikae kimya upatapo sintofahamu juu ya lishe ya mtoto wako ama wa ndugu jamaa na jirani yako! Tupigie simu namba 116 tuzungumze!

0 views
bottom of page