top of page
  • C-Sema Team

#SimuliziZa116: Baraka na Jose waunganishwa na mama yao Tarime

I

likuwa majira ya saa tatu asubuhi siku ya Ijumaa tarehe 15 Juni 2018 tulipopokea simu kutoka kijiji cha Nkende wilaya Tarime. Sauti ya mama ilisikika upande wa pili kwa masikitiko makubwa ikitueleza kupatikana kwa watoto wawili wa kiume, Baraka mwenye umri wa miaka saba na mdogo wake Jose, mwenye umri wa miaka mitatu.

Baraka na Jose (majina yao halisi tumeyahifadhi) walitekezwa pembezoni mwa barabara alfajiri ya siku hiyo. Walipoulizwa nyumbani kwao walikotoka hawakuwa na majibu na hata habari ya waendako hawakuijua.

Mama huyu mteja wetu (mtoa taarifa) alitueleza kuwa baada ya mahojiano ya kina na watoto hawa, mosi alibaini majina yao na pili kuwa Baraka ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Nkende. Alitueleza kwamba kwa kuwa aliijua namba 116 kwani aliwahi kuisikia redioni, aliona atupigie tupate kutoa msaada.

Watoto walieleza kuwa baba yao aliwaacha bila kuwaambia wapi anaenda. Baraka alisema, 'Mama na baba yetu waligombana jana usiku na alfajiri baba alituamsha na kuondoka na sisi hadi hapa alipotuacha, hatujui alikokwenda'. Tulimshauri mtoa taarifa hii kwenda Ofisi za Serikali ya Kijiji Nkende ambapo alituunganisha na Mwenyekiti wa Kijiji tuliyemshauri awapeleke watoto hao shuleni Nkende kwani walimu wake Baraka wanaweza kumtambua na kusaidia kuwatambua wazazi wa watoto hao.

Shuleni Nkende hatimaye waalimu walimtambua Baraka kama tulivyobashiri na hivyo waalimu kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Kijiji walimpata Mama Baraka na hivyo akaja kuwachukua watoto wake. Mwenyekiti wa Kijiji alitufikishia salaa za shukurani toka kwa Mama Baraka kwa zoezi hili la kusaidia kupatikana wa watoto wake.

Tunaendelea kuchagiza kuwa Huduma ya Simu kwa Mtoto inapatikana kote nchini kwa kupiga simu namba 116 bila malipo na imewaunganisha wazazi na watoto wao kama Mama Baraka. Inahitaji kuwiwa tu kama mama (mtoa taarifa) huyu aliyetupigia kutuletea habari hiki. Ingawa alipoteza kiasi fulani cha muda wake, mama huyu mwema leo hii anafarijika kwa kujua kwamba kupitia simu yake watoto Baraka na Jose wako katika mikono salama.

Tupigie simu namba 116 tuzungumze!

0 views

Comments


bottom of page