top of page
  • Writer's pictureNadhira Jiddawi

#SimuliziZa116: Baba asaini makubaliano kutoa matunzo kwa watoto baada ya talaka


Huduma ya Simu kwa Mtoto Zanzibar tulipokea simu kutoka kwa mama wa watoto watatu wenye umri wa miaka mitano (5), mitatu (3) na wa mwisho mwenye umri wa miezi kumi (10) pekee. Mama huyo mkazi wa shehia ya Dunga, wilaya ya Kati Unguja na alipiga simu kutoa lalamiko kwamba mumewe wa zamani ametelekeza wajibu wa kuwalea watoto wao.


Ni takriban miezi mitatu sasa tangu tulipotengana, mpaka sasa mwenzangu haleti chochote kwa ajili ya watoto! Natekeleza majukumu yote peke yangu ingawa yeye anao uwezo wa kuyatekeleza kwa kuwa anafanya kazi katika kampuni ya ujenzi. Alieleza mama huyo.


Aidha aliongeza kuwa anachohitaje yeye ni mwenza wake huyo wa zamani kuwajibika katika kutoa chakula, sabuni, nepi na nguo kwa ajili ya watoto.


Tulimtafuta baba wa watoto hao kabla ya kuiwasilisha kesi hiyo kwa Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya. Baba huyo alikanusha mashtaka hayo kutoka kwa mkewe wa zamani na kudai kwamba tangu walipotengana amekua akitoa matunzo kwa watoto wake, kinyume na alivyoripoti mtalaka wake. Hata hivyo, tulimjuza baba huyo juu ya uwasilishwaji wa kesi hiyo katika ngazi ya wilaya akapate kujibu mashtaka hayo yanayomkabili.


Afisa Ustawi wa Jamii pamoja na mama walirudisha mrejesho kwamba baba huyo alikubali wito wa kufika katika ofisi za wilaya na sasa anatoa matunzo kwa watoto kulingana na makubaliano yaliyotiwa saini chini ya usimamizi wa Afisa Ustawi wa Jamii yanayotamka kuwa baba huyo atatoa kiasi cha shilingi 150,000 kila mwezi kwa ajili ya matunzo ya watoto wake.


Tusikae kimya tukijua matukio kama haya yanaendelea mitaani, shehiani na vitongojini mwetu. Wasiliana nasi kupitia nambari 116 bila malipo tuzungumze.

1 view

Comments


bottom of page