top of page
Writer's pictureNadhira Jiddawi

#SimuliziZa116: Aolewa na alombaka kuficha aibu ya familia (muhali)

Mnamo Februari 14, 2019, Huduma ya Simu kwa Mtoto Unguja tulipokea simu kutoka kwa binti akiomba msaada kulipa bili ya matibabu ya mtoto wa kiume wa dada yake ambaye amekuwa akiugua kwa miezi takribani 10 sasa. Mtoto huyo alizaliwa na tatizo la kuvuja kwa mkojo ndani ya mwili - tatizo linalomsumbua mpaka leo.



Binti huyo alitupa kisa cha namna dada yake alivyopata ujauzito. Alisema kwa bahati mbaya wao ni yatima na toka wakiwa watoto wadogo wamelelewa na jirani mama msamaria mwema na mwenye moyo wa kujitolea. Walipopevuka yeye alianza kufanya kazi za nyumbani kama #mfanyakazi katika nyumba za majirani kujipatia kipato huku dada yake akimsaidia mama yao kazi za kutunza nyumba (kufua, kuosha vyombo, nk.).


Siku moja, mwanamume jirani aliyekuwa akiwatembelea hapo nyumbani kwao na hata kupiga soga na mama yao alipita na kugundua dada mtu aliachwa nyumbani pekee yake. Alimbaka na bahati mbaya zaidi alipata ujauzito. Tukio hilo liliripotiwa kwa mama na wanafamilia waliketi na kumtaka mtuhumiwa ajieleze. Alikiri kosa na kupendekeza kuwa anataka kumuoa dada mtu. Familia zilifikia makubaliano (muhali) na ndivyo dada mtu aliolewa.


Toka siku aliyoondoka nyumbani akiwa bibi harusi aliwekwa kwa dada wa mumewe. Mumewe huyo aliondoka kwa muda mrefu bila ya mawasiliano na baadaye dada wa mume alianza kumwambia kuwa mimba sio ya ndugu yao. Alipitia vurugu nyingi wakati wa ujauzito katika nyumba hiyo hatimaye aliamua imetosha na alirudi nyumbani. Wiki chache baadaye alimzaa mtoto mgonjwa ambaye ni mgonjwa tangu wakati huo.

Tuliripoti kisa hiki cha kusikitisha kwa Afisa wa Ustawi wa Jamii ambaye alimwita huyo mume. Mume alifika akiongozana na familia yake - wote walikataa kuwa ujauzito ule wamegundua si wa kwao na hivyo matunzo ya mtoto hayawahusu. Afisa Ustawi aliagiza kipimo cha DNA kifanyike huku akipeleka kesi hii mahakamani. Kesi hiyo bado inaendelea mahakamani.


Wasichana wengi wamepoteza ndoto za maisha yao katika mikono ya majirani, ndugu na jamaa. Ni wakati wa kuchukua hatua sasa - hakuna sababu ya kuendekeza muhali kuficha nyuso za wanafamila. Piga simu 116 kutoa taarifa za udhalilishaji dhidi ya wasichana na wanawake. Inaanza na wewe!

1 view
bottom of page