top of page
  • C-Sema Team

Siku ya Mtoto wa Afrika – 2020


Juni 16, 2020 – Dar es salaam.

Shirika la C-Sema kwa kushirikiana na Apps&Girls, Jamii Forums pamoja na Elimika Wikiendi, Children’s Dignity Forum, JengaHub, Msichana Initiative, Save the Children, Action Aid na Global Religions for Children Foundation kwa pamoja waliandaa maadhimisho ya #SikuYaMtoto wa Afrika mtandaoni mwaka huu kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Corona uliokwamisha uwezekano wa Watoto kukutana ana kwa ana.


Mwaka1991, wakuu wa nchi wanachama wa iliyokuwa OAU (sasa AU) walianzisha #SikuYaMtoto wa Afrika (DAC) kama kumbukumbu ya uasi dhidi ya wanafunzi uliotokea tarehe 16 Juni 1976 huko Soweto, Afrika Kusini. Wakati huo, wanafunzi waliandamana dhidi ya elimu duni ya kibaguzi waliyopewa na serikali ya kibeberu na kuomba kufundishwa kwa lugha zao wenyewe.


#SikuYaMtoto hutumika kuwakumbusha watoto wetu hatua ya kijasiri waliyoichukua wenzao huko Afrika Kusini katika kulinda haki zao. Watoto wanakumbushwa kwamba wanaweza kuleta mabadiliko hata wakiwa wadogo. Kwahiyo, #SikuYaMtoto inaadhimishwa kwa maslahi mapana ya watoto wa Afrika na inatupasa sisi watu wazima kujitolea kwa hali na mali katika nafasi zetu ili kushughulikia changamoto nyingi zinazowakabili watoto katika bara zima na hasa hapa nyumbani.


Tunakumbushana kuwa ili kuondokana na lindi la umasikini, ipo haja ya kuhakikisha 'hakuna mtoto anayeachwa nyuma' kwa kuongeza nguvu ili kuwafikia watoto hasa wale wasiofaidika na kukua kwa maendeleo ya Tanzania. Hivyo, kanuni kuu ni maendeleo ya pamoja kwa watoto, yaani, wakati wowote wa kuandaa mipango na sera za kutekeleza mipango mbalimbali, watoto wanapaswa kuwa ndani ya mipango ili 'kuhakikisha kwamba hakuna mtoto anaachwa nyuma' katika kuleta maendeleo ya uchumi endelevu. Hii ni muhimu hasa katika mazingira ya Tanzania ambapo watoto huunda idadi kubwa ya wananchi.


Mwaka huu tutawasikiliza watoto wakijadili mada ‘Haki na wajibu wa mtoto, upi ni wajibu wa wazazi, walezi na jamii?’ Mjadala huu utahudhuriwa na watoto wapatao 15 ambao watakuwa meza kuu wakiwakilisha maeneo mbalimbali. Kati ya hao watoto watano watatoka Pemba. Watano wengine watatoka Mbozi na watano wa mwisho watatoka Dar es salaam.


Takribani watoto wengine wengi watahudhuria kama hadhira mtandaoni ikiwa ni mara ya kwanza siku hii kuadhimishwa mtandaoni. Zuri Zaidi ya yote ni kuwa mtandao utakaotumika umetengenezwa na mabinti na watoto wadogo wa hapa hapa nyumbani Tanzania kutoka shirika la Apps&Girls lenye makao yake Jijini Dar es salaam.


Maadhimisho haya pia yamewakutanisha wazazi wenye Watoto wadogo wenye umri wa miaka 0 – 8 kuzungumza na kubadilishana uzoefu juu ya malezi ya watoto wadogo. Mjadala huu pia utahudhuriwa na wataalamu wa masuala ya saikolojia ya malezi na wawakilishi wa mashirika yanayotoa huduma kwa watoto hapa Tanzania. Wazazi wengine kote majumbani waliruhusiwa kuingia katika mjadala huu kama hadhira.


Mwisho maadhimisho haya pia yaliwapa fursa watoto wenye kupenda uchoraji kupata darasa toka kwa mchoraji mahiri aliyetoa darasa la uchoraji kwa watoto mtandaoni. Mamia ya watoto walijiunga na darasa hilo.


Tunatumia maadhimisho haya ya #SikuYaMtoto kuwakumbusha viongozi, wananchi na vyombo vya habari kuwa maendeleo ya taifa letu hayawezi kupiga hatua bila kutilia maanani mahitaji ya watoto, ikiwa ni pamoja na watoto masikini na walio na mazingira magumu zaidi kutengewa mafungu toka katika bajeti kuu ya serikali na zile za halmashauri.


Tukumbushane kwamba gharama ya kutokufanya chochote ili kubadili hali ya watoto wetu ni kubwa mno. Kushindwa kuwekeza katika huduma muhimu na ulinzi wa watoto wote sio tu kunawanyima watoto haki zao lakini kutaingiza gharama kubwa zaidi kwa Taifa baadaye kwa ajili ya maisha tegemezi watakayoishi, kupoteza na kupunguza uzalishaji.


Watoto wanapaswa kuchukuliwa kama mawakala wa mabadiliko kwani zaidi ya nusu ya wakazi wa Tanzania ni watoto. Ili walau wajukuu na vitukuu vyetu vipate kuishi kwa neema lazima tuanze na maisha ya watoto wetu sasa. Wapate elimu bora, afya njema, chakula na malazi safi. Kwa kuwekeza kwa watoto sasa, Tanzania itaziba pengo kubwa la umasikini na kiasi kikubwa cha watu wazima wa miaka 2030 na zaidi wataishi maisha yenye neema. Tuanze kujibu hitaji hili sasa.


Yapo mafanikion tuloyafikia katika miongo miwili iliyopita mfano viwango vya kuandikishwa na mahudhurio ya shule sasa yako juu, Tumepunguza idadi ya vifo vya watoto, tumeongeza upatikanaji wa huduma za msingi kama afya kwa watoto na kuongeza idadi ya watoto wa kike wanaoendelea na masomo, miongoni mwa lundo la mafanikio mengine.


Hata hivyo, umakini unapaswa kuongezwa kwa kutambua idadi kubwa ya watoto walio katika mazingira magumu ambao ‘huachwa nyuma' au ambao ‘huishi pembezoni’ katika maeneo mbalimbali nchini. Hawa ni pamoja na watoto wenye ulemavu, watoto yatima, wasichana na watoto waishio katika maeneo ya vijijini.


Yafuatayo nimaeneo ya kutilia nguvu kama taifa:

  1. Tujipange kumaliza njaa na utapiamlo kwa watoto; kuhakikisha upatikanaji wa chakula salama, chenye uwiano wa lishe bora kwa ukuaji wa miili na bongo za watoto wetu; tushughulikie mahitaji ya lishe ya wanawake wajawazito na wenye kunyonyesha; na kupambana na tatizo sugu la udumavu wa watoto nchini.

  2. Tukatae watoto wetu wachanga kufa vifo vinavyoweza kuzuilika kwa kuongeza uwekezaji katika huduma za afya ya uzazi kwa kina mama wanaojifungua katika kliniki zetu.

  3. Hakikisha kuwa wasichana na wavulana wote wanamaliza elimu ya msingi, na kuwa wote wanajiunga sekondari na kwamba wote wanao uwezo sawa kujifunza na kupata matokeo mazuri.

  4. Kujenga na kuboresha majengo ya shule ili yaingilike na kutumika kwa watoto wenye ulemavu, viwepo vifaa maalumu kwa ajili ya watoto wenye ulemavu na uwekezaji makini kupata walimu wenye weledi kufundisha watoto wenye ulemavu.

  5. Kwa kiasi kikubwa tupunguze aina zote za ukatili kwa watoto; ukatili wa kingono, vipigo, ajira za kinyonyaji kwa watoto #WAFANYAKAZI, tupunguze biashara za aina zote zinazowatumia watoto kama kitenga uchumi kingono, nk.; kukuza utawala wa sheria na kuhakikisha upatikanaji sawa wa haki kwa watoto wote, ikiwa ni pamoja na watoto wenye mahitaji maalumu.

  6. Tuhakikishe upatikanaji wa maji safi na salama kwa watoto wote na pawepo usawa katika upatikanaji wa maji safi kwa wote, mijini na hata vijijini; usafi wa kutosha majumbani na mashuleni na utumiaji wa vyoo na pawepo vyoo mashuleni na hata majumbani vyenye usafi.

  7. Tuhakikishe miundo mbinu ya usafiri na makazi yanafikika kwa watoto wote, pawe salama na ya gharama nafuu hasa usafiri kwa watoto wa mijini wanaotumia usafiri wa uma kwenda shule.

1 view

Comments


bottom of page