top of page
C-Sema Team

Mtoto Josephine (jina halisi limehifadhiwa) atolewa katika ndoa na kurudi shuleni.


Mnamo tarehe 10 Januari mwaka 2019 jirani mmoja kutoka wilayani Hai kata ya Bondeni alipiga simu Kituo cha Huduma ya Simu kwa Mtoto kupitia namba 116 na kutoa taarifa zilizomhusu binti wa miaka 12 aliyetambulika kwa jina la Josephine.


Jirani huyo alieleza kuwa, Josephine alifanikiwa kumaliza darasa la saba mnamo mwaka 2018 na matokeo yalivyotoka akafanikiwa kupata ufaulu mzuri wa kujiunga na elimu ya sekondari ingawa wazazi wake walimua kumuozesha kwa mwanaume mtu mzima aliyemzidi umri badala ya kumpeleka binti shule.


Mara moja, Kituo cha Huduma ya Simu kwa Mtoto kilitoa taarifa ya kesi hiyo kwa Afisa Ustawi wa jamii wa eneo lililotokea tukio na kwa usaidizi wa jirani aliyetoa taarifa wahusika wote walikamatwa na mtoto akatenganishwa na mumewe huyo sambamba na kuandikishwa shule ili aendelee na masomo. Baada ya miezi kadhaa kupita, Kituo cha Huduma ya Simu kwa Mtoto kilipata kuwasiliana na Mwalimu Mkuu katika shule ambayo Josephine aliandikishwa, nae akakiri kumpokea binti huyo na kueleza kuwa tayari ameanza kuingia darasani kwa ajili ya kuendelea na masomo.

Visa vya kuwakatisha mabinti walofaulu kuendelea na masomo yao kwa sababu za ndoa viko lukuki. Usiishie kulalamika tu. Chukua hatua, tupigie namba 116 bila malipo na kwa usiri mkubwa tutashirikiana na mamlaka za serikali kunusuru maisha ya mtoto husika. Inaanza na jirani. Jirani ni wewe.

1 view
bottom of page