top of page
  • C-Sema Team

Maadhimisho ya siku ya mtoto wa afrika na umuhimu wake kwa watoto


Mwaka 1991, wakuu wananchi wanachama wa OAU walianzisha Siku ya Mtoto wa Afrika (DAC) kama kumbukumbu ya uasi dhidi ya wanafunzi 16 Juni 1976 huko Soweto, Afrika Kusini. Wakati huo, wanafunzi watoto wadogo waliandamana, mosi kupinga aina ya elimu duni ya kibaguzi waliyopea na serikali ya kibeberu, pili waliitaka serikali ya mzungu iwape ruksa kufundishwa kwa lugha zao wenyewe.


Siku ya Mtoto wa Afrika hutumika kuwakumbusha watoto wetu hatua ya kijasiri waliyoichukua wenzao huko Afrika Kusini katika kulinda haki zao. Watoto wanakumbushwa kwamba wanaweza kuleta mabadiliko hata wakiwa wadogo. Kwa hivyo, Hivyo #SikuYaMtoto inaadhimishwa kwa maslahi mapana ya watoto wa Afrika na inapaswa sisi watu wazima kujitolea kwa hali na mali katika nafasi zetu ili kushughulikia changamoto nyingi zinazokabili watoto katika bara zima na hasa hapa nyumbani.


Mwaka huu tunakumbushana kuwa ili kuyafikia Malengo Endelevu ya Agenda ya 2030, ipo haja ya kuhakikisha kwamba 'hakuna mtoto anayeachwa nyuma' kwa kuongeza nguvu ili kuwafikia watoto hasa wale wasiofaidika na kukua na maendeleo ya Tanzania. Hivyo, kanuni kuu ni maendeleo ya pamoja kwa watoto, yaani, wakati wowote wa kuandaa mipango na sera za kutekeleza Agenda 2030, watoto wanapaswa kuwa ndani ya mipango ili 'kuhakikisha kwamba hakuna mtoto anaachwa nyuma' katika kuendesha maendeleo ya uchumi endelevu. Hii ni muhimu hasa katika mazingira ya Tanzania ambapo watoto huunda idadi kubwa ya wakazi wake.


Wazazi watambue kuwa familia ndio taasisi ya kwanza kuweka msingi wa maendeleo ya watoto kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa yaliyosainiwa na mataifa yaliyo mengi duniani, ikiwemo Tanzania. Mataifa yanapokaa na kukubaliana malengo kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watoto humaanishi kuwa serikali na wadau wamaendeleo wanao wajibu kuyatekeleza, lakini zaidi sisi wazazi na jamii kuanzia katika ngazi ya familia nasi tunayo sehemu ya kutekeleza. Vinginevyo familia zetu zitaachwa nyuma.


Takwimu za kituo cha Huduma ya Simu kwa Mtoto, zinaonyesha watoto wamekuwa wakipitia magumu ikiwemo vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, utelekezwaji, vipigo, utumikishwaji wa kazi ngumu, mimba na ndoa za utotoni ambapo yote haya yanakatiza ndoto zao za kimakuzi na mendeleo. Vitendo hivi hufanywa na ndugu zetu, jamaa zetu na sisi wenyewe wazazi. Namna hii mchango wetu katika maendeleo ya watoto wetu ni hasi. Hawawezi kushindana na watoto wanaolelewa katika mataifa yaloamka, mathalani Uchina na kwingineko. Tunaweza kubadili hili kwa kuongeza umakini katika malezi ya watoto wetu.


Tunatumia maadhimisho haya ya Siku ya Mtoto wa Afrika kuwakumbusha viongozi, wananchi na vyombo vya habari kuwa maendeleo ya taifa letu hayawezi kupiga hatua bila kutilia maanani mahitaji ya watoto, ikiwa ni pamoja na watoto masikini na walio na mazingira magumu zaidi ktengewa mafungu toka katika bajeti kuu ya serikali na zile za Halmashauri.

Tukumbushane kwamba gharama ya kutokufanya chochote ili kubadili hali ya watoto wetu ni kubwa mno. Kushindwa kuwekeza katika huduma muhimu na ulinzi wa watoto wote sio tu kunawanyima watoto haki zao lakini kutaingiza gharama kubwa zaidi baadaye kwa ajili ya maisha tegemezi watakayoishi, kunapoteza na kupunguza uzalishaji.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

1 view

Comments


bottom of page