Alhamisi Novemba 2, 2023 Dar es salaam.
Leo Kamishna wa Ustawi wa Jamii nchini Dkt. Nandera Mhando amefanya kikao-kazi katika ofisi za Kituo cha Huduma kwa Mtoto. Kikao-kazi hili kililenga kufanya mapitio ya awali ya uandaaji wa huduma ya Afya ya Akili na Saikolojia (MHPSS - Bot) inayotarajiwa kuanza kutumika kupitia jumbe fupi za maneno (SMSes / USSD), pamoja na mitandao ya WhatsApp, Telegram n.k.
Picha: Katikati ni Dkt. Nandera Mhando Kamishna Ustawi wa Jamii akiwa na Kiiya JK, Mtendaji Mkuu C-Sema (kushoto) na Mtakwimu wa Huduma ya Simu kwa Mtoto, Bi. Beatrice Kessy (kulia).
Kamishna Dr. Mhando amejiridhisha kuwa kazi iliyofanyika kwa maandalizi ipo katika hatua nzuri na ameshauri namna bora ya utekelezaji wa huduma hiyo na kuangazia jinsi itakavyoshughulikia mahitaji ya kisaikolojia ya watoto nchini.
Kikao hiki pia kilihudhuriwa na jopo la wataalamu wa ulinzi wa mtoto na ubunifu (UNICEF Innovation) lililoongozwa na Mkuu wa Idara ya Ulinzi wa Mtoto UNICEF Tanzania, Bi. Maud Droogleever Fortuijn. Shirika na UNICEF ni mbia muhimu katika uandaaji wa huduma hii ya MHPSS-Bot.
Picha: Mkuu wa Idara ya Ulinzi wa Mtoto UNICEF Tanzania, Bi. Maud Droogleever Fortuijn na Mkuu wa Kitengo cha Ubunifu UNICEF Tanzania Ndugu Nelson Rodrigues wakiwa katika umakini wa kikao cha mapema leo.
Katika ziara hiyo, Kamishna Dkt. Mhando na ujumbe wake sambamba na wawakilishi kutoka UNICEF walifanya mapitio ya kina kuhusu huduma ya MHPSS-Bot, malengo yake, na namna itakayotumika kutoa msaada wa afya ya akili kwa watoto na vijana. Kikao hicho pia kilijadili umuhimu wa kujumuisha usaidizi wa afya ya akili na saikolojia katika mipango mipana ya ulinzi wa mtoto. Kamishna Dkt. Mhando hakusita kueleza dhamira ya serikali ya kuunga mkono na kuimarisha programu ya MHPSS ili kuhakikisha watoto wanapata msaada muhimu wa afya ya akili na saikolojia.
Picha: Waote walipata fursa ya kuangalia MHPSS-Bot inavyofanya kazi.
Kikao pia kilitoa jukwaa la mazungumzo na ushirikiano kati ya serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, C-Sema, na UNICEF.
Kamishna aliambatana na mtaalamu wa Afya ya akili toka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Bi. Lillian Masuha.
Imeandaliwa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
C-Sema
Comments