Mwaka mpya unatoa nafasi nzuri ya kutafakari mambo yaliyopita na kupanga kwa ajili ya yajayo. Hii siyo tu kwa watu wazima bali pia kwa watoto. Kama wazazi, huu ni wakati muafaka wa kuimarisha uhusiano na watoto wetu kwa kuzungumza nao, kuonesha mshikamano wa kifamilia, na kutanabaisha maadili yanayoongoza familia zetu.

Kwa mujibu wa utafiti wa Chama cha Madaktari wa Watoto Marekani (AAP), watoto wanaoishi katika familia zinazoweka mawasiliano wazi na kufuata maadili thabiti huwa na ustawi wa kihisia na kijamii wa hali ya juu. Hivyo, tuanze mwaka huu kwa kuzungumza na watoto wetu, kuelewa mahitaji yao, na kujenga misingi imara ya kukuza na kuendeleza maadili ya familia.
Kama wazazi, tunaweza kufanikisha hili kwa kuwauliza watoto maswali rahisi na yenye maana yatakayowasaidia kutafakari kuhusu maisha yao na kuimarisha uhusiano baina yetu. Mfano;
Ni kitu gani kilikufurahisha sana mwaka uliopita?
Swali hili linawasaidia watoto kutafakari mambo mazuri yaliyowatokea na kuwajenga kuwa na mtazamo wa shukrani. Ikiwa mtoto amesema alipenda kushinda mashindano shuleni, tunaweza kutumia fursa hiyo kumpongeza na kumtia moyo kufanya vizuri zaidi.
Ni jambo gani ulitamani lingekuwa tofauti mwaka jana?
Hii ni fursa ya kuzungumzia changamoto zao na kufikiria njia za kuzitatua mwaka huu. Mtoto akisema alihisi upweke wakati fulani, tunaweza kujadili njia za kumsaidia asijiskie hivyo.
Ungependa kujifunza au kujaribu kitu gani kipya mwaka huu?
Swali hili linahamasisha udadisi na kuwasaidia kuweka malengo mapya kwa mwaka 2025. Ikiwa mtoto angependa kujifunza kucheza mpira wa miguu, masuala ya teknolojia au kuchora, tunaweza kujitahidi kupanga ratiba ya mafunzo pamoja naye ili kumuwezesha kufikia ndoto zake.
Nawezaje kuwa mzazi bora kwako mwaka huu?
Swali hili linaonesha kuwa tunathamini maoni ya watoto wetu, jambo linalojenga uaminifu na heshima. Mtoto akisema angependa tuongeze muda wa kucheza naye, kusoma naye, kufanya matembezi nk. tunaweza kupanga siku maalum za kufanya hayo
Ungependa tufanye nini kama familia mwaka huu?
Shughuli za kifamilia huimarisha mshikamano na kuunda kumbukumbu nzuri za pamoja. Hivyo maoni ya mtoto kwenye hili yakizingatiwa yataimarisha uhusiano na ushirikiano wa familia.
Pamoja na kwamba maswali haya yanawasaidia watoto kuutafakari mwaka uliopita na kujiandaa na mwaka huu, maswali haya pia hujenga nafasi ya kutafakari maadili gani tunataka watoto wetu wjifunze mwaka huu wanavyozidi kukua pamoja na kujitathmini mwenendo wetu wa malezi kama wazazi . Kama tunavyofahamu, maadili ya familia ni dira inayoelekeza mwenendo wa kila mmoja katika familia. Ni muhimu kuyahuisha ili kuhakikisha kila mtu anayaelewa na kuyatekeleza.
Tuzungumze na watoto wetu na kuwauliza kama wanafahamu familia yao inasimamia misingi gani ya maadili. Majibu yao yanaweza kutuonesha mtazamo wao na kuanzisha mjadala. Tukiwa tunazungumza nao tujitahidi kutafsiri maadili tunayotaka kuwafundisha kwa maneno rahisi sana sana kwa watoto wadogo. Mfano, “kuwa mkweli” au “kusaidiana” yanaweza kufafanuliwa kwa mifano rahisi kama; "Ukimuahidi rafiki yako kitu, ni muhimu kukitimiza." au "Leo tutashirikiana kufua nguo na kupika chakula cha usiku." Na kuhakikisha mambo hayo yanatekelezeka.
Ili Watoto waweze kuyaishi maadili haya inatupasa kuyafanya sehemu ya mwenendo wa maisha ya familia zetu. Tunaweza kufanya hivyo kwa kutengeneza ratiba au shughuli mfano, kila Ijumaa inaweza kuwa ni siku ya shukrani, ambapo tunakaa na watoto wetu kuzungumza nao kuhusu umuhimu wa shukrani na hata kuwauliza katika wiki ni jambo gani ambalo wanashukuru lilitokea.
Mazungumzo ya wazi kama hayo yanawawezesha watoto kujihisi salama kihisia hivyo kuyashika maadili hayo kwa urahisi. Utafiti wa Harvard Center on the Developing Child unaonesha kuwa watoto wanaopata msaada wa kihisia kutoka kwa wazazi huwa na ustahimilivu mkubwa wanapokutana na changamoto.
Tunaweza kuimarisha mawasiliano na watoto wetu ili kuwa na mazungumzo ya wazi kwa kuwapa watoto nafasi ya kusema wanachohisi bila kuwakatisha au kuwahukumu. Tunaweza kuewaelezea changamoto zetu binafsi au malengo yetu ya mwaka mpya, uwazi wetu kwao utawafanya wawe wazi kwetu. Mfano: "Mwaka jana nilipitia changamoto kazini, kazi zilikua nyingi, lakini nilijifunza kupanga muda wangu vizuri zaidi." Na kama tulivyoeleza hapo juu tuweke ratiba maalumu kila wiki ya kuwa na mazungumzo ya kifamilia ili kila mtu awe na nafasi ya kueleza mawazo yake.
Haya yote tuliozungumza leo ni muhimu kwa sababu yanaimarisha uwezo wa watoto wa kuelewa hisia zao na za wengine, jambo linalochangia ustawi wa kijamii. Pia, Jarida la Saikolojia ya Familia (The Journal of Family Psychology) linaonesha kuwa familia zinazoimarisha maadili na kuwasiliana vizuri hujenga kizazi cha watoto wenye ujasiri na maadili mema.
Tujiulize leo, familia zetu zina misingi ya maadili ipi na ni mambo gani tungependa kuwafundisha watoto wetu.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org