top of page

Mzazi anza kumjengea mwanao tabia ya kujitegemea mapema

C-Sema Team

Tunapata wasiwasi mkubwa juu ya maisha ya baadaye ya watoto wetu kwamba watakuwa na maisha ya aina gani? Watakuwa watu wazima wa namna gani? Hivi watafanikiwa kielimu? Biashara? Kimsingi, sisi wazazi ndiyo watu pekee wenye jukumu la kuhakikisha kuwa tunalea watoto wetu katika namna ambayo tungependa wawe kama usemi wa wahenga usemao 'mtoto umleavyo ndivyo akuavyo'.


Tabia ya kujitegemea kwa kiasi kikubwa huja kutokana na msukumo wa wazazi na namna makuzi yanavyotolewa. Anza kwa kumpa fursa mtoto kujifanyia vitu au mambo madogo-madogo kadiri anavyozidi kukua. Aanze kujua dhana ya kunawa mikono pekee yake kuanzia umri wa miaka mitatu au mapema zaidi. Mweleze kwa nini kunawa mikono ni muhimu.


Mfunde kuoga pekee yake mapema. Aanze kufua nguo nyepesi kama kanga au shati la shule mapema. Taratibu ajue akitoka shule pana kazi kadha wa kadha zinazomsubiri. Mtie moyo kwa kumsifu pindi anapojaribu kujifanyia jambo mwenyewe pasi kuambiwa. Hii itamfanya aendelee kujihusisha na jambo hilo mara kwa mara na mwishowe atavuna uzoefu katika hilo.

Heshimu mawazo ya mtoto. Watoto wetu hupenda sana kutoa maoni yao kama sehemu ya utatuzi wa changamoto za siku hata siku katika familia zetu. Zungumza na mtoto wako, kubaliana naye lakini mpe sababu kwa nini unajua anachoshauri hakiwezekani. Unamjengea uwezo wa kusimama pekee yake katika hoja. Mpe fursa ya kuchagua nguo anayopenda kuvaa haya mambo madogo yanatafsiri ya uhuru wa kuamua. Huku nako ni kukuza dhana ya kujitegemea.


Upo ushahidi wa kutosha kuwa baadhi ya wazazi huwafanyia watoto wao kila kitu majumbani mwao. Dhana ya kwamba wanawapenda sana. Lakini swali la kujiuliza ni kuwa je, utaishi na watoto wako maisha yao yote? Mapenzi kwa watoto ni pamoja na kuwaandalia kesho yao kupitia kazi kama kufagia nyumba kufuta vumbi madirishani, kuosha vyombo, kutandika kitanda, n.k Mpe usaidizi wa maswala ambayo dhahiri ni magumu kwake. Namna ya kukabiliana na msiba, changamoto za kielimu, namna ya kujenga uhusiano bora wa kirafiki na watoto wengine, kuwaheshimu wakubwa, n.k. ni baadhi ya mambo ambayo yanahitaji ukaribu na miongozo ya kutoka kwako mzazi. Mtambulishe kwa ndugu wa familia tandaa apate kujenga mahusiano na shangazi zake, wajomba zake, bibi na babu pasi wewe kuingilia-ingilia. Awasiliane nao binafsi kadiri anavyokua.

Bahati mbaya sana wazazi hasa wa mijini tunatumia muda wetu mwingi kazini na hata tunaporudi majumbani hatutaki watoto wetu wamsaidie mfanyakazi wa nyumbani kazi. Kwani tunalea bianadamu au mwanasesele? Tena mtoto akianza kupata marafiki anaaambiwa akome. Ataishi vipi dunia hii bila kuhusiana na binadamu wengine? Uzoefu wa kuwa na marafiki tabia za watu mbalimbali na mambo namna hii hawezi kupata ndani ya nyumba yako. Malezi ya watoto ni jambo lenye kuhitaji subira na uvumilivu. Muamini mtoto. Hatokuangusha.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org

0 views
bottom of page