top of page
C-Sema Team

Ijue nafasi ya wazazi na watoto katika kurithi mali za wapendwa wao.

Wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya mahakama siku chache zilizopita tulishuhudia mama mmoja akidai haki yake na watoto katika kurithi mali anazodai aliachiwa na marehemu mume wake. Tukio hili lililozua mijadala lukuki katika mitandao ya kijamii linatusukuma kutaka kujua sheria za Tanzania zinasemaje juu ya urithi na wosia wa marehemu. Je, zipi taratibu za kufuatwa wakati wa kugawa mali za marehemu? Makala haya yatajikita katika taratibu za kisheria katika mirathi.


Urithi ni mali aliyoacha marehemu kwa ajili ya kupewa watu wenye haki ya kuzipata (warithi wake halali). Sheria za mirathi ndio zinazoongoza ukusanyaji, uangalizi, usimamizi, ugawaji na umiliki wa mali za marehemu, pamoja na kulipa madeni aliyoacha marehemu wakati wa uhai wake au gharama zitokanazo na mazishi yake. Awepo mtu ambaye atazisimamia na kuzigawa kwa wahusika wakiwamo wadai kuepusha mgongano katika jamii husika.



Sheria zinazohusu urithi na wosia (mirathi) hapa Tanzania zipo za aina tatu ambazo ni; Sheria ya Serikali, Sheria ya Mila na Sheria ya Dini ya Kiislam. Sheria ya Serikali inatokana na Sheria ya Urithi ya India ya mwaka 1865. Sheria hii ilianza kutumika nchini India tangu mwaka 1865 lakini ililetwa Tanzania (wakati huo Tanganyika), na Serikali ya Wakoloni wa Kiingereza. Sheria hii inaongoza na kusimamia mgawanyo wa mali za marehemu pale ambapo itaonekana kwamba marehemu alikuwa hafuati Sheria za Kiislam wala Sheria za Kimila au kama ni waislamu hawataki sheria ya dini yao kutumika katika mirathi.


Mgawanyo wa mali kwa kutumia sheria hii ni mjane atapata 1/3 na watoto 2/3 ya mali zote za marehemu. Iwapo marehemu hakuacha watoto, basi mjane atapata ½ ya mali na nyingine inayobaki hugawanywa sawasawa kati ya wazazi, kaka, na dada wa marehemu. Mgawanyo wa mali kwa mujibu wa Sheria ya Serikali hufanyika pale tu ambapo marehemu hakuacha wosia. Kama kuna wosia mali zitagawanywa kwa mujibu wa wosia. Vilevile sheria hii haiwapi haki ya kurithi mali watoto wa nje ya ndoa isipokuwa tu kama upo wosia unaowarithisha mali.


Sheria ya Mila hutumika kwa wananchi wote wa Tanzania ambao si wa asili ya Asia, Ulaya au Wasomali na ambao katika maisha yao walifuata taratibu au sheria za kimila (mila na desturi za kabila lake). Ikiwa sheria ya kimila itatumika, urithi hufuata upande wa ukoo wa kiumeni. Warithi huwa ni watu wanaoangukia katika vyeo vya aina tatu; cheo daraja la kwanza hiki hushikwa na mtoto wa kiume wa kwanza kutoka katika nyumba ya kwanza (kama ilikua ndoa ya wake wengi), au mtoto wa kiume aliyezaliwa kwanza kutoka nyumba yoyote - iwapo marehemu hakuacha mtoto wa kiume katika nyumba ya kwanza. Cheo daraja la pili hushikwa na watoto wote wa kiume waliosalia ambao hurithi sehemu kubwa kuliko watoto wa kike ambao huhesabika kama daraja la tatu.


Cheo daraja la tatu ndio cha mwisho na kinajumuisha watoto wa kike wote bila kujali tofauti ya nafasi ya mama zao katika ndoa. Hawa hupata sehemu ndogo kuliko watoto wa kiume. Lakini kama watoto wa kiume hawapo basi watoto wa kike huongezewa urithi. Hata hivyo ni muhimu ieleweke kwamba Zingatio Sheria ya ardhi ya vijiji ya mwaka 1999 ilisahihisha utaratibu wa umiliki ardhi wa kimila (urithi wa ardhi) kwa kuondoa ubaguzi wa aina zote kwenye umiliki wa ardhi na kuweka usawa kwa wanawake na wanaume. Sheria hiyo ya Ardhi inazibatilisha sheria zote za kimila zinazowanyima wanawake, watoto au watu wenye ulemavu uhalali wa kumiliki mali, kutumia au kupata ardhi. Hivyo cheo cha tatu cha urithi kwenye sheria za kimila kinakuwa batili pale urithi wa mali ya marehemu unapogusa suala la ardhi (wanaume na wanawake watagawana sawa ardhi ya urithi).


Sheria ya mila inawanyima wajane haki ya kurithi mali za marehemu waume zao. Kwamba mjane mwenye watoto inabidi aishi kwa kutegemea watoto wake. Mjane ambaye hana watoto atabaki katika nyumba ya marehemu na kupewa asilimia 20 ya nusu ya mali ya marehemu na kuitumia wakati wa uhai wake. Akifariki au akiolewa na mtu mwingine nje ya ukoo mali hiyo na nyumba aliyokuwa anakaa hugawiwa kwa warithi halali wa marehemu mume wake. Vilevile sheria hii inamnyima mume haki ya kurithi mali za mke wake katika urithi usio na wosia, isipokuwa pale tu ambapo mke hakuacha watoto na hakuacha kabisa mtu yoyote katika ukoo wake. Wanasheria na wanaharakati wengi wanakubaliana kuwa sheria hii kwa sasa inakosa uhalali wa Kikatiba kwa kuwa haki za binadamu zinataka usawa bila ya ubaguzi.


Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org


15 views
bottom of page