Uhalisia ni kwamba fimbo ambayo mara nyingi imekua ikizungumziwa kwenye Biblia kama fimbo anazotakiwa kupewa mtoto ili kumjenga ni fimbo ya mchungaji kwa ajili ya kuongozea kondoo, au fimbo ashikayo kiongozi wa familia kumtofautisha na wanafamilia wengine. Mfano hai ni fimbo aliyoitumia Musa katika kugawanya bahari ya Shamu ama fimbo aliyonyooshewa malkia Esta na mfalme ambayo inaweza leta uhai ama kifo. Kwa tafsiri ya kawaida mtu hudhani ni fimbo ndogo nyembamba lakini kwa tafsiri ya Kiebrania fimbo hii ni sawa na shina la mti unaochipua.
Kiebrania ni lugha yenye mawanda mapana sana na hivyo imesababisha lugha hii iwe na ugumu hasa kwenye tafsiri kutoka Kiebrania kwenda lugha nyingine za kimagharibi kama Kigiriki ama Kiingereza. Mamlaka aliyonayo mtu yalionyeshwa na alama ama kito kilichopatikana juu ya fimbo yake. Mathalani mtu aliyehitaji hifadhi aliangalia alama juu ya fimbo walizokuwa nazo wenyeji wake na mara moja alitambua mwenye mamlaka ya juu. Huyu ndiye mwenye uwezo wa kutoa hifadhi, pia alikua msemaji wa koo ama kabila. Huyu ndiye alipewa mamlaka ya kufundisha vijana na watoto wa koo za familia.
Torati ilieleza na kutoa mipaka ya matumizi ya fimbo na hakuna mahali iliongelea juu ya upigaji wa mtoto au kueleza namna mtoto apigwe. Ilieleza namna ya kupiga mjakazi ama mtumwa na maeneo ya kupigwa. Mipaka hii ilikua ni kwa ajili ya kuzuia watu kulewa madaraka na madhara yake. Kutoka 21:20 inaeleza kuwa, 'Na ikiwa mtu atampiga mtumwa wake au kijakazi wake kwa fimbo naye kwa kweli afe chini ya mkono wake lazima na yeye atalipiwa kisasi.' Hivyo watu waliogopa kwenda kinyume na Torati.
Sasa, tuyageukie maandiko ambapo tukianzia mstari ule wa Methali 23:12 unasema kuwa, 'Tumia akili zako kufuata mafundisho, tumia maskio yako kusikiliza maarifa.' Methali 23:13-14, 'Usiache kumrudi / kumuonya mtoto, ukimchapa kiboko hatakufa. Ukimchapa kiboko utayaokoa maisha yake na kuzimu. Maneno kama 'kuonyooka' na 'kuchapa kiboko' hayana uhusiano wa moja kwa moja na maana ya kumpiga mtoto kwa fimbo.
Wazazi wa Kiebrania walilea watoto wao kwa kufuata Torati na kanuni zake zote. Walihakikisha watoto wao wanakua na busara, ufahamu na adabu njema kwa kuielewa Torati. Torati haikuongelea matumizi ya fimbo kwa mtoto hivyo hawakuitumia kuadhibu watoto. Kitu pekee ambacho fimbo iliwakilisha ni mamlaka aliyonayo baba juu ya mtoto na kwamba mamlaka yale yaliwakilishwa na fimbo ilojaa mawaidha na busara anazopaswa kumfundisha mtoto wake.
Kama maana ya fimbo itokanayo na Torati imeeleweka basi ni rahisi kuelewa kuwa fimbo kwa mtoto haijawahi kuwa fundisho kwa mzazi wa Kiebrania. Kupiga kwa mtoto huua busara, hekima, upendo hata uelewa juu ya mambo mbalimbali yahusuyo tabia na namna afanye ili kuepuka kurudia kosa. Wanafilosofia wa Kigirikii waliamini sana juu ya kupiga viboko na hivyo maandiko haya waliyaelewa kumaanisha hivyo. Hata tafsiri tulizopokea awali zilipelekea sisi Waswahili kudhani viboko vinatokana na maelekezo ya Biblia jambo ambalo tumeona si kweli.
Maana halisi iko wazi, hasa juu ya neno 'kipigo' na neno 'fimbo.' Waebrania wakiwa kama wafuasi wa Torati wasingeruhusu mtoto kuchapwa hasa na fimbo ilhali wanaelewa kuwa madhara yatokanayo na kipigo ni kifo. Mkanganyiko unatokana na walio wengi kuisoma Biblia kwa tafsiri moja na bila kuitafakari na kuelewa. Fimbo inayozungumzwa hapa ni kama tulivyoona awali, ni sawa na shina la mti unaochepua. Ni ishara ya uongozi na maarifa.
Ni majukumu ya kufundisha watoto ili wafuate Torati na maandiko. Je wangeruhusu vipi itumike kumchapia mtu? Kama Methali 23 ingekua inamaanisha kuchapwa na fimbo basi vifungu vingine vinavyofuata vingekua ni ulaghai. Kana kwamba isingekua hatia kwa mzazi kuua mtoto wake kwa fimbo na kumuokoa nafsi yake na umauti.
Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116 ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
ความคิดเห็น